Mashirika ya kutetea haki za wanawake nchini Afrika Kusini, yalielezea ghadhabu yao Alhamisi na kuwakosoa Polisi kwa kudhaniwa kuwa wameshindwa, baada ya mashtaka kufutwa dhidi ya wanaume 14, wanaotuhumiwa kwa ubakaji .
Wanaume hao pia wanashutumiwa kwa kuwaibia wanawake waliokuwa wakitengeneza filamu, katika mgodi uliotelekezwa wa Krugersdorp, magharibi mwa Johannesburg.
Waendesha mashtaka wa serikali walisema hakuna ushahidi wa kutosha dhidi ya watu hao ili kuendelea na kesi hiyo.
Wanaume hao wanaoaminika kuwa wachimba migodi haramu, walikamatwa wakati wa msako wa polisi katika mgodi huo baada ya wanawake wasiopungua wanane kuvamiwa na kubakwa walipokuwa wakirekodi video ya muziki mwezi Julai.
Ripoti za ubakaji huo zilizua maandamano ya vurugu katika vitongoji karibu na Krugers-dorp huku wananchi wakiwashutumu wachimbaji wadogo wanaofanya kazi katika shimo la migodi iliyotelekezwa kwa kufanya uhalifu huo.
Waandamanaji hao pia walishuka kwenye migodi hiyo iliyotelekezwa, na kuzuia mashimo ya wachimbaji hao kwenda chini ya ardhi na kuchoma mahema yao ya muda na mali zao. Wachimba migodi hao walikamatwa, kushambuliwa na kukabidhiwa kwa polisi.