Akifungua kongamano hilo, kiongozi wa Baraza la Waislamu wa Amerika ya Kaskazini ICNA, Dk. Mohsin Ansari ametoa wito kwa waislamu kuungana ili kukabiliana na chuki dhidi ya waislamu inayoongezeka kote duniani.
Anasema imani na siasa za itikadi kali zinatishia jamii zote na kuna haja ya watu kufanya kazi kwa pamoja kuwaelimisha na kuwaongoza juu ya namna ya kuishi pamoja.
Wajumbe elfu 22 wanaohudhuria kongamano hilo wanashiriki kwenye majadiliano, warsha, mikutano na mashindano katika fani mbali mbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa familia kuwa pamoja, masuala ya afya, namna ya kuimarisha biashara na uchumi miongoni mwa waislamu pamoja na jukumu la wanawake na vijana katika jamii.
ICNA yenye makao makuu yake mjini Chicago ina idara zinazoshughulikia elimu, afya, vijana, wanawake, huduma za dharura, huduma za familia, makazi kwa wahamiaji pamoja na juhudi za kuzuia njaa.
Katika kongamano la Baltimore wajumbe wamezingatia zaidi changamoto zinazowakabili vijana hii leo Marekani ikiwa upande wa elimu, manyanyaso, matumizi ya dawa za kuelvya pamoja na kukosa miongozo mizuri kuhusiana na imani yao ya kislamu.
Dk. Ansari ametoa wito kwa familia kuwafuatilia watoto wao na kuwapatia elimu na muongozo wa dini yao ya kislamu kutokana na changamoto za maisha na mazingira wanazokabiliana nazo hapa Marekani.
Mbali na mikutano na mijadala, kuna soko kubwa kwenye ukumbi mkuu wa jengo la mkutano ambapo wafanyabiashara wa kislamu kutoka sehemu mbali mbali za Amerika Kaskazini wamepata fursa kuuza bidhaa zao na kujitangaza.