Mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa Waislamu ulianza Jumamosi katika baadhi ya nchi kote duniani huku maeneo mengine yakitarajia kuanza saumu hiyo siku ya Jumapili.
Shirika la habari la AP linaripoti kwamba katika nchi nyingi kote duniani, wengi walikuwa na matumaini ya kuuanza mwezi huu wa Ramadhan kwa furaha hasa baada ya janga la virusi vya corona, ambapo takriban Waislamu bilioni 2, hawakuweza kwenda kuhiji Makka, kwa miaka miwili mfululizo. Lakini licha ya matumaini hayo,
uvamizi wa Russia nchini Ukraine, umepelekea mamilioni ya watu katika sehemu mbalimbali duniani kufadhaika, hasa kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa, ambako kunaathiri zaidi watu wanaoishi kwenye maeneo yenye migogoro, ikiwa ni pamoja na nchi kama Lebanon, Iraq, Syria, Sudan na Yemen.
Vita nchini Ukraine vimeongeza makali hayo kwa kuwa nchi hiyo pamoja na jirani yake, Russia, ni wazalishaji wa theluthi moja ya ngano inayotegemewa na nchi kadhaa duniani kuwalisha mamilioni ya watu wake. Russia na Ukraine pia ni wauzaji wakubwa wa nafaka nyingine, pamoja na mafuta ya alizeti yanayotumika kwa kupikia, ambayo uhaba wake unashuhudiwa katika nchi nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.