Vifaru 24 wameuawa nchini Afrika kusini katika muda wa wiki mbili.
Wizara ya mazingira imesema kwamba mizoga ya vifaru saba imepatikana katika mbuga ya kitaifa ya Wanyama ya Kruger, saba mengine katika mkoa wa Mpumalanga, sita KwaZulu-Natal na nne imepatikana Western Cape.
Wizara hiyo imelaani uwindaji haramu wa vifaru kwa ajili ya kupat apembe zao, ikisema kwamba washukiwa tisa wamekamatwa ndani ya siku 14 za mwezi Desemba.
Wizara hiyo imewashawishi raia wa Afrika kusini kutoa taarifa zozote zinazoweza kuwasaidia maafisa kuwakamata wawindaji haramu.
Afrika kusini ina karibu asilimia 80 ya vifaru 30,000 walio kote Afrika
Mamia ya vifaru huuawa kila mwaka kwa pembe zao zinazouzwa nchi za Asia na kutumika kutengeneza dawa.
Wizara ya mazingira ya Afrika kusini imesema kwamba itatoa taarifa zaidi kuhusu idadi ya vifaru ambao wameuawa mwaka 2021, mapema mwaka 2022.