Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 06:01

Dr Fauci anasema Omicron inaweza isiwe kali kama Delta lakini uchunguzi zaidi unahitajika


Mshauri mkuu wa rais wa Marekani, Joe Biden, kwenye masuala ya afya Dr Antony Fauci, amesema Jumapili kwamba ingawa virusi vipya vya corona vya Omicron vinaenea kwa haraka, uchunguzi uliofanywa kufikia sasa unaonyesha kwamba huenda visiwe hatari kuliko vilivyotangulia kama vya delta.

Dr Fauci wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha CNN kwenye kipindi cha State of the Union hata hivyo amesema kwamba wanasayansi wanahitaji kufanya utafiti zaidi kabla ya kutoa ripoti ya uhakika kuhusu Omicron.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, ripoti kutoka Afrika kusini ambako virusi hivyo viligunduliwa siku kadhaa zilizopita kwa mara ya kwanza, zinasema kuwa idadi ya wagonjwa waliolazwa hospitali kutokana na maambukizi haijaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Dr Fauci ameongeza kusema kwamba utawala wa Biden unatadhmini kuondoa marufuku yaliyowekwa dhidi ya wageni wanaoingia hapa Marekani iwapo sio raia, kutoka mataifa kadhaa ya kiafrika.

Marufuku hiyo iliwekwa muda mfupi baada ya kugundulika kwa Omicron ingawa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyakemea mataifa yaliyochukua hatua hiyo, akiitaja kama ya kibaguzi kwa usafiri.

Kufikia Jumapili, virusi vya Omicron vilkuwa vimeripotiwa kwenye takriban theluthi moja ya Marekani yakiweno majimbo ya Wisconsin na Missouri ambako kesi za karibuni kabisa zimeripotiwa.

Ripoti zinaongeza kusema kwamba virusi vya awali vya Delta bado vinaongoza kwenye idadi ya maambukizi hapa Marekani wakati timu za wanajeshi zikitumwa New York na Massachusetts ambako wagonjwa wengi wamelazwa hospitalini.

Maafisa wa afya wa Marekani wameendelea kuwasihi watu kupata chanjo pamoja na ile ya ziada ya booster,wakati wakiendelea kuzingatia kanuni za kuvaa barakoa, pamoja na kuweka umbali unaohitajika, ili kujiepusha na maambukizi.

XS
SM
MD
LG