Maafisa wa serikali ya Ethiopia wamehimiza raia kujitayarisha kulinda makao yao, baada ya wapiganaji wa Tigray, ambao wamekuwa wakipiga vita serikali kuu kwa mda wa mwaka mmoja sasa, kutangaza kwamba wataingia katika mji mkuu Addis Ababa.
Kulingana na shirika la habari la Ethiopia, viongozi wa mji wa Addis Ababa, wametaka raia kusajili silaha zao na kukusanyika tayari kwa mapambano.
Utawala wa Addis umesema kwamba msako wa nyumba hadi nyumba unaendelea mjini humo ili kuwakamata watu wanaopanga kuzua fujo.
Raia wametakiwa kujikusanya katika mitaa wanayoishi ili kujilinda na wale walio na silaha lakini hawataki kujihusisha katika kulinda sehemu wanazoishi, wametakiwa kusalimisha silaha zao kwa serikali au watu wa karibu wa jamii zao au marafiki.
Televisheni inayomilikiwa na serikali ya Fana, imetangaza kwamba serikali imehimiza raia kujikusanya na kupigana na kundi la Tigray.
Msemaji wa kundi la TPLF Getachew Reda amesema kwamba iwapo wapiganaji wa Tigray na washirika wake wanafanikiwa kuondoa madarakani serikali iliyopo, wataunda serikali ya mpito.
Amesema kwamba majadiliano ya kitaifa yatafanyika lakini Waziri mkuu Abiy Ahmed na mawaziri wake hawatashiriki katikamajadiliano hayo.
Mzozo wa Ethiopia ulianza Nove 3 2020, wapiganaji wa TPLF waliposhambulia kambi ya jeshi ya Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
Katika kujibu shambulizi hilo, Waziri mkuu Abiy Ahmed alituma wanajeshi kadhaa eneo hilo na kuanza mashambulizi dhidi ya wapiganaji.
Kundi la TPLF limedhibithi siasa za Ethiopia kwa karibu miongo mitatu lakini likapoteza umaarufu Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwaka 2018 baada ya miaka kadhaa ya maandamano ya kupinga serikali.