Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 06, 2023 Local time: 06:30

Tigray watishia kuingia Addis kuangusha serikali, Raia wahimizwa kuwa tayari kupigana


Moshi baada ya shambulizi la bomu katika mji wa Mekele, mji mkuu wa eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, Oct. 20, 2021.
Moshi baada ya shambulizi la bomu katika mji wa Mekele, mji mkuu wa eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, Oct. 20, 2021.

Maafisa wa serikali ya Ethiopia wamehimiza raia kujitayarisha kulinda makao yao, baada ya wapiganaji wa Tigray, ambao wamekuwa wakipiga vita serikali kuu kwa mda wa mwaka mmoja sasa, kutangaza kwamba wataingia katika mji mkuu Addis Ababa.

Kulingana na shirika la habari la Ethiopia, viongozi wa mji wa Addis Ababa, wametaka raia kusajili silaha zao na kukusanyika tayari kwa mapambano.

Wito wa viongozi wa Addis Ababa, umetolewa baada ya wapiganaji wa kundi la Tigray People liberation Front TPLF, kudai kwamba wamedhibithi miji kadhaa katika siku za hivi karibuni na kwamba wanapanga kuingia kwa mguu katika mji mkuu wa Addis Ababa, ulio umbali wa kilomita 380 kutoka mahali walipo.

Utawala wa Addis umesema kwamba msako wa nyumba hadi nyumba unaendelea mjini humo ili kuwakamata watu wanaopanga kuzua fujo.

Raia wametakiwa kujikusanya katika mitaa wanayoishi ili kujilinda na wale walio na silaha lakini hawataki kujihusisha katika kulinda sehemu wanazoishi, wametakiwa kusalimisha silaha zao kwa serikali au watu wa karibu wa jamii zao au marafiki.

Televisheni inayomilikiwa na serikali ya Fana, imetangaza kwamba serikali imehimiza raia kujikusanya na kupigana na kundi la Tigray.

Msemaji wa kundi la TPLF Getachew Reda amesema kwamba iwapo wapiganaji wa Tigray na washirika wake wanafanikiwa kuondoa madarakani serikali iliyopo, wataunda serikali ya mpito.

Amesema kwamba majadiliano ya kitaifa yatafanyika lakini Waziri mkuu Abiy Ahmed na mawaziri wake hawatashiriki katikamajadiliano hayo.

Mzozo wa Ethiopia ulianza Novemba 3 2020, wapiganaji wa TPLF waliposhambulia kambi ya jeshi ya Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Katika kujibu shambulizi hilo, Waziri mkuu Abiy Ahmed alituma wanajeshi kadhaa eneo hilo na kuanza mashambulizi dhidi ya wapiganaji.

Kundi la TPLF limedhibithi siasa za Ethiopia kwa karibu miongo mitatu lakini likapoteza umaarufu Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwaka 2018 baada ya miaka kadhaa ya maandamano ya kupinga serikali.

Vita vya Ethiopia vimepelekea zaidi ya watu 400,000 kukosa chakula katika eneo la Tigray, maelfu kuuawa na zaidi ya watu milioni 2.5 kukimbia makwao.

Mjumbe maalum wa Marekani katika pembe ya Afrika Jeffrey Feltman, amesema kwamba Washington imeshtushwa na kuzorota kwa hali ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia na kutaka pande husika kutafuta mbinu za kumaliza mzozo huo, Pamoja na kuruhusu msaada kuwafikia waathiriwa.

Jeffrey Feltman amesema kwamba Marekani inaona dalili za kutokea janga kubwa la chakula na kwamba serikali ya Ethiopia inazuia msaada kuwafikia waathiriwa.

Serikali ya Ethiopia hata hivyo imekanusha madai ya kuzuia msaada kufika sehemu hiyo.

XS
SM
MD
LG