Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 05, 2024 Local time: 15:56

Viongozi wa kanisa Uganda wanataka uchaguzi uahirishwe. Museveni aongezewe miaka 3 zaidi


Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Muungano wa makanisa nchini Uganda unataka katiba ya Uganda kufanyiwa marekebisho na kusitisha uchaguzi wa Januari 14 ili kumruhusu rais Yoweri Museveni kuendelea kuwa madarakani kwa mda wa miaka 3 zaidi.

Muungano huo umesema kwamba mazingira ya sasa nchini humo hayaruhusu kufanyika uchaguzi huru na haki.

Wakiongozwa na askofu mkuu wa kanisa katoliki Uganda Dkt Cyprian Kizito Lwanga, viongozi wa makanisa yote Uganda wanasema kwamba katiba ya nchi hiyo inastahili kufanyiwa marekebisho na uchaguzi kuahirishwa kutokana na janga la virusi vya Corona.

Wamesema kwamba wamefikia hatua hiyo baada ya majadiliano ya mda mrefu, yaliyoangazaia janga la virusi vya Corona na hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa nchini Uganda, wakisema kwamba mazingira ya sasa hayawezi kufanikisha uchaguzi ulio huru na haki.

Katika kikao na waandishi wa habari jijini kamapla, Dkt Lwanga amesema kwamba bunge linastahili kuchukua hatua za haraka na kufanyia marekebisho katiba ya nchi na kuongeza mda wa utawala wa sasa kwa miaka mitatu zaidi.

Kulingana na viongozi hao wa makanisa, wanasiasa hawafuati kanuni za maafisa wa afya namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona na hivyo kuwepo ongezeko la maambukizi na vifo.

Wamekosoa maafisa wa usalama kwa kile wametaja kama kuwakandamiza wagombea wa upinzani, kuwakamata, kuwazuia kufanya kampeni, kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya mikutano ya kampeni na kuwapiga wafuasi wa upinzani.

Kulingana na katiba ya Uganda, uchaguzi unapoahirishwa, spika wa bunge anastahili kuongoza serikali.

Ibara ya 259 ya katiba ya Uganda inatoa fursa kwa bunge kufanyia marekebisho katiba, na viongozi hao wa makanisa wanataka mabadiliko kufanyika ili Museveni aendelee kuongoza nchi hiyo.

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo, amesema kwamba mapendekezo ya viongozi hao yamepitwa na wakati.

Zimealia karibu wiki tatu, Uganda kuandaa uchaguzi mkuu, Januari 14 mwaka ujao 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA,Washington DC

XS
SM
MD
LG