Mara tu baada ya Odinga kula kiapo hicho katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilitoa ilani kuwa vuguvugu la NRM linaloongozwa na kiongozi huyo wa upinzani ni kikundi cha wahalifu. Ilani hii ilitolewa kwenye gazeti rasmi la serikali.
Hatua hiyo ya serikali ya Kenya ilionekana kama hatua za haraka kutaka kutokomeza vuguuugu la ukombozi linaloongozwa na Bw Odinga linalojulikana kama National Resistance Army.
Odinga alikula kiapo katika bustani ya Uhuru Park na kusisitiza kupambana na dhuluma zinazotokana na ulaghai wa kura. Serikali ya Kenya kupitia ilani iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali inaeleza kuwa kwa mujibu wa kipengee cha 22 cha sheria ya 2010 inayodhibiti uhalifu nchini Kenya.
George Musamali, mtaalam wa usalama nchini Kenya aliambia Sauti ya Amerika kuwa hatua hiyo ya serikali huenda ikazalisha kikundi kingine cha kijeshi kinachomtii Bw Odinga.
Na japo Afisa Mkuu Mtendaji wa NASA Norman Magaya kupitia ujumbe wa Twitter ameeleza kuwa NRM si shirika wala kundi bali ni wazo tu na hivyo basi serikali haiwezi kuidhibiti.
Odinga aliapishwa katika hafla ya iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi na kueleza kuwa uapisho wake ni mwanzo wa mageuzi makubwa nchini Kenya.
Na japo Bw Odinga alishindwa kueleza kile kinachofuata baada ya kula kiapo, kilichokuwa dhahiri ni kukosekana kwa washirika wake,Kalonzo Musyoka,Moses Wetangula na Musalia Mudavadi. Lakini kwa taarifa kwa vyombo vya habari, watatu hao wameeleza kuwa ilikuwa vigumu kwao kukutana na kufanya mkutano kwa sababu ambazo hawengeweza kuziepuka na kusisitiza kuwa watakutana wote chini ya siku mbili kushauriana.