Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 10:25

Upinzani Kenya wamchagua Odinga kuwania urais


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Raila Odinga amechaguliwa kupeperusha bendera ya upinzani katika kinyang'anyiro cha uchaguzi nchini Kenya. Mgombea huyu amewahi kutumikia nafasi ya waziri mkuu katika serikali ya Kenya.

Muungano wa vyama vya upinzani (NASA) nchini Kenya umesema Alhamisi umemchagua kiongozi huyo mzoefu wa upinzani kuwa mgombea Urais katika uchaguzi utaofanyika Agosti 8 mwaka huu.

Odinga, mwenye umri wa miaka 72 atapambana na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anagombea kwa awamu ya pili kuongoza tena kwa miaka mitano.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa wagombea hawa wawili ndio walipambana katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwaka 2013.

Amesema kuwa aidha muungano huo umetangaza mpangilio wa mgao wa mamlaka endapo utashinda katika uchaguzi huo. Kiongozi wa Wiper Demokratic Movement, Kalonzo Musyoka, atakuwa mgombea mwenza huku vinara wengine watatu kwenye muungano huo, wakipewa nyadhifa mbali mbali za ngazi za juu, endapo wataibuka washindi tarehe nane mwezi Agosti.

Makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi alisema wakati atanamtangaza Odinga, viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.

Orodha ifuatayo ndiyo iliyotangazwa:

  • Raila Odinga - Mgombea urais
  • Kalonzo Musyoka - Mgombea mwenza
  • Musalia Mudavadi - Waziri Mkuu
  • Moses Wetangula - Naibu Waziri Mkuu
  • Isaac Ruto - Naibu Waziri Mkuu

"Hii ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito," alisema Bw Odinga akihutubu baada ya kutangazwa kuwa mgombea.

Amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.

"Sisi tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu".

Alisema serikali yake itaangazia kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kurejesha gharama ya elimu na maisha chini.

Bw Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari,pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.

Kadhalika, ameahidi akishinda serikali yake itamaliza rushwa serikalini.

Akitangaza orodha ya nyadhifa hizo, liyejkuwa wakati mmoja makamu wa rais Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.

"Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa," amesema,” alisema Mudavadi.

Muungano huo wa NASA ulifanya mkutano wake katika bustani za Uhuru Park, mjini Nairobi.

Hayo yanajiri huku chaguzi za mchujo, kuwatafuta wagombea wa nyadhifa mbali mbali, watakaowakilisha vyama vya kisiasa, zikiendelea kufanyika nchini kote.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu BMJ Muriithi, Washington DC

XS
SM
MD
LG