Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 19:57

Makadirio ya bajeti ya Kenya: Mikate na unga yaondolewa ushuru


Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Katika bajeti ya tano ya madaraka ya Bwana Kenyatta, shilingi bilioni 14 na 33 zimetengewa elimu ya bure ya msingi pamoja na ile ya upili mtawalia.

Waziri wa Fedha nchini Kenya Henry Rotich amekuwa mbioni kuulezea bayana mkakati wa Rais Uhuru Kenyatta wa kudhibiti hali mbaya ya maisha ambayo imekuwa ikiwakumba wakenya wengi. Katika maduka mbalimbali, bei za bidhaa za kimsingi zimeonekana kuwa ghali mno na kuwafanya wakenya kulalamikia hilo.

Sasa katika bajeti hii ambayo imeelezea kwa kina mikakati ya kufadhiliwa kwake, serikali imeeleza kutovitoza ushuru vifaa maalum vinavyotumiwa katika hospitali, magari yanayotengezwa nchini humo kufanikisha shughuli za utalii, vifaa vinavyotumika kutengeneza dawa za kuwaua wadudu, vifaa muhimu vinavyotumika kutayarisha mifuko ya samaki pamoja na mikate ya kawaida na kuapa kuhakikisha haya yanatekelezwa.

Waziri wa fedha wa Kenya Henry Rotich amesema "Mkate wa kawaida na unga wa mahindi havitozwi ushuru kumaanisha kuwa havipokei faida ya punguzo la thamani. Na ili kufanya bidhaa hizi kuwa nafuu kwa mkenya wa kawaida napendekeza kuondoa ushuru kwa mkate na unga wa mahindi na kuondoa ushuru kwa pamoja. Wazalishaji na wauzaji wa bidhaa hizi wanafaa kupunguza bei ya bidhaa hizo la sivyo nitabatilisha sheria."

Katika bajeti ya tano na ya mwisho katika awamu ya kwanza ya madaraka ya Bwana Kenyatta, shilingi bilioni 14 na 33 zimetengewa elimu ya bure ya msingi pamoja na ile ya upili mtawalia. Ili kufanikisha uchaguzi mkuu utakaoandaliwa Agosti nane mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 21.4 za ziada kwa tume huru ya uchaguzi na kufikisha kiasi cha mfuko wa IEBC kuwa shilingi bilioni 40.7.

Aidha, serikali pia inapendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya kodi ya mapato na ili kuwatoza ushuru watu wanaopata mapato ya shilingi 13,483 huku Tume ya Kupambana na Ufisadi EACC ikitengewa shilingi bilioni 2.3.

Lakini huku utawala wa Jubilee ukipanga kutekeleza bajeti ya shilingi trilioni 1.7 kutokana na ushuru na shilingi bilioni 900 kutoka mikopo na misaada, baadhi ya wakenya wanaeleza kutoridhika.

XS
SM
MD
LG