Mahakama mmoja mjini Nairobi Kenya imewaachilia huru raia wawili wa Iran na Mkenya mmoja baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kukubali raia hao warejeshewe makwao mara moja.
Mwandishi wa VOA Nairobi, Kennedy Wandera ameripoti kwambaSayed Ebrahimi na mwenzake Abdolhosein,raia wa Iran pamoja na dereva wao Moses Mmboga ambae ni Mkenya walipatikana Novemba mosi na picha na video za Ubalozi wa Israeli kwenye simu zao na kuwekwa kizuizini.
Katika uamuzi wake siku ya Jumatan, Hakimu Joyce Gandani aliamuru serikali kuwarejesha makwao raia hao mara moja.
Uamuzi huu ulifikiwa baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa palikuwa na maafikiano kati ya Kenya na Ubalozi wa Iran nchini juu ya kuwarejesha raia makwao.
Ni wiki mbili tangu raia hao wa kigeni na Mkenya kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa tuhuma za kupiga picha katika ubalozi wa Israel jijini Nairobi
Baadae walifikishwa kizimbani kuelezea kilichowashawishi kupiga picha na kunasa video za ubalozi huo.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Duncan Ondimu aliieleza mahakama kuwa watatu hao walikuwa na nia mbaya na kuwa ni tishio kwa taifa.
“Wakati taifa limekuwa likikabiliwa na matukio ya ugaidi ambayo tayari yameathiri taifa kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Lakini wakili anaewatetea watuhumiwa hao watatu, Ahmednassir Abdullahi aliitaka mahakama kupuuzia mbali madai ya serikali.
Kwa mujibu wa mwandishi wa VOA wiki iliyopita watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani na kuomba wapewe dhamana lakini walikataliwa kwa maadai ya upande wa mashtaka kwamba mwenendo wao ni hatari kwa taifa.
Wakati huo huo uamuzi wa mahakama umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wakenya.
Kwa mujibu wa Dunstan Omari ambae ni wakili wa Mahakama Kuu nchini kunaweza kukawa na mtafaruki iwapo Waisraeli wanaamini wale raia wa Iran walikuwa wanapiga picha kwa nia ya kuchunguza ubalozi wao.
Lakini aliongeza kuwa Kenya inataka uhusiano mzuri na mataifa yote na hivyo inauhusiano wa kidiplomasia na Isreali na Iran bila kuzibagua.
Mwaka 2015 raia wa Iran walikamatwa na kukutikana na hatia ya kosa la ugaidi ambapo walihukumiwa kifo.
Lakini hukumu hiyo baadae ilipunguzwa hadi miaka 15.