Mapigano makali kati ya maafisa wa usalama wa Uganda na walinzi wa mfamle wa kijadi na wanamgambo wanaotaka kujitenga katika jimbo la magharibi la Rwenzori yamesababisha vifo vya watu 54 Jumapili asubuhi.
Msemaji wa polisi wa Uganda, Felix Kaweesi amesema maafisa 13 wa polisi na wanamgambo 41 waliuliwa Jumamosi katika mapigano makali katika wilaya ya Kasese wakati wanamgambo walipowashambulia polisi walokua wanapiga doria.
Kaweesi anasema maafisa wanne wa polisi na wanajeshi wanne wamejeruhiwa.
Mauwaji haya ni matokeo ya ugomvi wa muda mrefu kati ya vikosi vya usalama vya Uganda na walinzi wa mfalme wa kijadi Charles Wesley Mumbere mpinzani mkuu wa rais Yoweri Museveni.
Inaripotiwa Rais Museveni alimpigia simu mapema mfalme Mumbere kuvunja kundi la walinzi wake, kabla ya kukamatwa na kusafirishwa na polisi hadi Kampala hii leo.
Mumbere ni mfalme wa himaya ya Rwenzururu, na baadhi ya wafuasi wake wamekua wakitoa wito wa kutaka kujitenga kutoka Uganda. Mfalme amekanusha kua na jukumu lolote katika mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi.
Jimbo la magharibi ya Uganda ambako Mumbare ana makazi yake, ni ngome kuu ya upinzani dhidi ya Rais Museveni, ambako alishindwa katika uchaguzi mkuu uliyopita.
Facebook Forum