Marais Hassan Shiekh Mohamud wa Somalia na Uhuru Kenyatta wa Kenya wamekubaliana kuondoa marufuku ya safari za miraa kutoka Nairobi hadi Mogadishu kuanzia Jumatano Septemba 14. Somalia ilipiga marufuku usafiri wa miraa mapema mwezi Septemba ikidai imechukua hatua hiyo kutokana na sababu za maslahi ya kitaifa.
Msemaji wa rais wa Somalia Daud Aweys, ameiambia Sauti ya Amerika kwamba viongozi hao wawili walikutana kando ya mkutano wa kihistoria wa viongozi wa IGAD huko Mogadishu siku ya Jumatano na kuzungumzia maswala mbali mbali ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zao mbili.
Aweys anasema, hivi sasa safari za ndege zitaondoka moja kwa moja Nairobi hadi Mogadishu bila ya kupitia Wajir, na hivyo kuimarisha usalama katika vinwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Mohadishu.
Mbali na usafiri wa miraa kamati maalum itaundwa kati ya nchi hizo kutayarisha mipango ya kuimarisha biashara, kuanzishwa huduma za fedha na kurahisisha usafiri wa raia kwa kupunguza masharti ya kupata visa.