Marekani inaadhimisha miaka 15 tangu mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 magaidi walipoteka ndege na kuzigongesha katika majengo ya World Trade Center mjini New York, na Pentagon mjini Washington. Ndege ya tatu ilianguka eneo la mashambani katika jimbo la Pennsylvania.
Rais Barack Obama ataadhimisha kwa muda wa kukaa kimya White House Jumapili kabla ya kuzungumza katika maadhimisho yatakayofanyika Pentagon - makao makuu ya jeshi la Marekani - kwa heshima ya waliouawa katika mashambulizi yale.
Watu waliofariki katika shambulizi la World Trade Center watakumbukwa kwa majina mjini New York.
"Miaka 15 iliyopita, siku ya Septemba iliyoanza kama nyingine ilikuja kuwa moja ya siku ya kiza kuliko zote katika historia ya taifa letu," Obama alisema Jumamosi katika hotuba yake ya wiki kwa njia ya radio.
Rais alisema karibu "watu 3000 wasio na hatia waliuawa" siku ile ya Septemba "kutoka kila aina ya maisha, rangi na dini zote na imani kutoka kote Amerika na kote duniani."
Obama alisema mengi yamebadilika katika miaka 15, lakini "ni muhimu pia kukumbuka kile ambacho hakijabadilika - thamini ambazo zitatufanya kuwa Wamarekani. Uvumilivu unaotufanya tusonge mbele....magaidi kamwe hawataweza kuishinda Marekani."
Akiandika katika ujumbe wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alisema "Siku ya 9/11, tunakumbuka wale tuliowapoteza, wale waliojaribu kuwaokoa. Tunawakumbuka kwa kuendelea kutafuta amani, usalama, haki duniani kote."