Baada ya aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Uganda generali David Sejusa kufikishwa kwenye mahakama ya kijeshi mjini Kampala Uganda, wakili wake Ladislaus Rwakafuzi amezungumza na Sauti ya Amerika na kudai kwamba serikali ya rais Yoweri Museveni ina njama za kumzuilia Gen Sejusa hadi baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.
Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 61, amefunguliwa mashtaka matatu yakiwemo kushiriki mikutano ya kisiasa kinyume cha sheria za jeshi la Uganda UPDF, kutofika kazini bila idhini pamoja na kutomtii mkuu wa majeshi.
Katika taarifa yake ya ufunguzi Jenerali Sejusa alisema hana tatizo kwa kesi yake kusikilizwa na wadogo wake licha ya kuwa ni kinyume cha sheria ya jeshi la nchi hiyo.
Mkuu huyo wa zamani wa ujasusi alikataa kukubali kama anakosa au la akisema, msimamo wake ni kwamba kuna kesi inayohusiana na hiyo mbele ya mahakama kuu ya nchi, na hivyo anataka sheria iheshimiwe.
Aliyesimamia kesi hiyo kama mwenyekiti aliamuru Jenerali Sejusa apelekwe katika jela ya Lukuzi ambako wahalifu sugu huwa wameshikiliwa.