Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 17:10

Nkurunziza ashikilia msimamo dhidi ya majeshi ya AU


Samantha Power, Balozi wa Marekani katika UN na Rais Nkurunziza wa Burundi wakizungumza na waandishi wa habari, Gitega, Burundi, Jan. 22, 2016.
Samantha Power, Balozi wa Marekani katika UN na Rais Nkurunziza wa Burundi wakizungumza na waandishi wa habari, Gitega, Burundi, Jan. 22, 2016.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza Ijumaa alirudi msimamo wake wa kupinga kuletwa kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika nchini mwake kurejesha hali ya usalama.

"Watu wameamua kupitia bunge la taifa," Rais Nkurunziza aliuambia ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaotembelea nchi hiyo. Alisema Umoja wa Afrika "ni lazima uheshimu Burundi kama nchi mwanacha na lazima ishauriwe" katika swala hilo.

Mwezi uliopita, Umoja wa Afrika ulitangaza utapeleka jeshi la askari 5,000 kulinda usalama Burundi kwa kipindi cha mwanzo cha miezi sita, kufuatia ghasia zilizokuja baada ya uchaguzi na kuuwa watu wasiopungua 439 tangu April na kusababisha wengine zaidi ya 220,000 kukimbia nchini humo.

Hali ya Burundi inatazamiwa kuwa swala muhimu viongozi wa nchi za Afrika watakapokutana wiki ijayo kwa ajili ya mkutano wao wa mwaka mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Rais Nkurunziza wa Burundi
Rais Nkurunziza wa Burundi

Wachambuzi wana hofu kuwa ghasia zilizochochewa na kile ambacho wengi wanakiona kama awamu ya tatu ya uongozi ya Nkurunziza kinyume na katiba zinaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya watu wa makabila ya Kitutsi na Kihutu - sawa na vile vilivyokumba nchi hiyo kutoka 1993 hadi 2005.

Nkurunziza hata hivyo amepuuzia wasiwasi wa kimataifa kuwa mauaji ya jumla, kama yale yaliyotokea Rwanda 1994, yanaweza kutokea Burundi.

Albert Shingiro, mwakilishi wa kudumu wa Burundi katika Umoja wa Mataifa ambaye alihudhuria mkutano wa ujumbe huo na Rais Nkurunziza, alisema alifurahishwa na matamshi ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power kuionya Rwanda isiingilie maswala ya Burundi.

Juhudi Zinaendelea

Power aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya zaidi ya saa mbili na Nkurunziza kuwa "hatukufanikiwa mengi, kwa kweli, kama ambavyo tungependa." Alisema, hata hivyo, baraza la usalama halitakata tamaa, " kwa sababu swala la amani Burundi ni muhimu mno kulikatia tamaa."

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekuwa wakiihimiza serikali ya Burundi kufanya mazungumzo yanayojumuisha pande zote katika upinzani.

Ijumaa, wajumbe hao pia walifanya mfululizo wa mikutano na vyama vya siasa, makundi ya kiraia na viongozi wa kidini ambao walikuwa na maoni yanayofanana na pande zote mbili - serikali na upinzani. Walikutana pia na kundi la wawakilishi kutoka kwa vyombo vya habari huru.

XS
SM
MD
LG