Huku muda ukiwa unamalizika kwenye mkutano wa ya hali hewa unaoendelea karibu na Paris, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameyasihi mataifa kuweka kando tofauti zao.
Kerry ametaka kufikiwa kwa makubaliano thabiti ambayo yataiweka sayari yetu kwenye njia bora endelevu.
Pia alitangaza kuwa Marekani itaongeza mara mbili misaada na kufikia dola millioni 860 kwa mataifa maskini ili kuyawezesha kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Huku saa chache zikiwa zimebaki kufikia makubaliano ya hali hewa waziri Kerry alihitimisha ujumbe wake kwa maneno machache kwa kusema, “Jukumu letu liko bayana. Wakati wetu ni huu, tuifanye kazi hii."
Wapatanishi sasa wana chini ya siku mbili kufikia makubaliano yanayolenga kuweka viwango vya hali ya joto la ulimwenguni mpaka degree mbili za "Celcius," au chini ya viwango kabla ya enzi ya viwanda.
Waziri wa mambo yanje wa Ufaransa Laurent Fabius ambaye anaongoza mazungumzo hayo amesema rasimu mpya iliyowasilishwa jana imepungua nguvu.
Amesema sasa kuna kurasa 29 badala ya 43 na makubaliano yanaonekana kukaribia kukubalika katika maeneo kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na upelekaji wa teknologia kwa mataifa maskini duniani.
Wajumbe hii leo wanakabiliwa na siku ya mwisho ya kufikia makubaliano ambayo yatapitishwa rasmi hapo kesho.