Umoja mataifa unapanuwa kambi ya wakimbizi ya Kakuma huko kaskazini mwa Kenya, ili kuweza kuhudumia mtiririko wa wakimbizi wanaotoroka ghasia huko Sudan Kusini. Takriban watu elfu 50 wamekimbilia Kenya katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita.
Hapo awali iliwahi kuwa makazi ya vijana waliojulikana kama “ The Lost Boys” ambao walitoroka vita Sudan kabla nchi hiyo haijagawanyika. Lakini kwa wakati huu, , kambi ya wakimbizi ya Kakuma,nchini Kenya, inapangwa kupanuliwa ili iweze kuwahudumia idadi inayoongezeka ya raia wa Sudan kusini wanaotoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa lao jipya.
Msemaji wa idara ya wakimbizi ya umoja mataifa UNHCR, Emmanuel Nyabera, anasema kabla ya mzozo huo kuibuka hapo mwaka 2013, maelfu ya wakimbizi walikuwa wanarudushwa makwao na kambi hio ikaanza kupunguka.
Nyabera anasema kambi hiyo ambayo kwa sasa inawahudumia wakimbizi takriban elfu 180, tayari imeshapitisha kiwango chake. Eneo jipya lilopangwa kuwahudumia wakimbizi elfu 80, wengi wao watahamishwa kutoka kambi waliopo sasa ili kupunguza msongomano.
Bw. Nyabera anasema kwamba kuna wakimbizi kutoka takriban mataifa 17 kwenye kambi ya Kakuma, ikiwa ni pamoja na wakimbizi kutoka somali,Eritrea na Congo. Lakini sasa wakimbizi kutoka Sudan kusini ndio wanaoongoza kwa wingi. Kwa baadhi yao hii si mara yao ya kwanza kuishi kwenye kambi ya Kakuma. Wengi walirudishwa makwao, ila iliwabidi kutoroka tena, mzozo mpya ulipoanza.
Vita vya Sudan kusini vimewapambanisha vikosi vitiifu kwa rais Salva Kiir dhidi ya waasi wanao muunga mkono makam rais wa zamani Riek Machar. Licha ya makubaliano kadhaa ya amani ambao yameshindikana, ghasia zimeongezeka. Idara ya watoto ya umoja mataifa UNICEF, hivi karibuni iliripoti kuwa takriban watoto 129 wameuwawa katika shambulizi la serikali mwezi ulopita, na makundi ya kutetea haki za binadam yamezishutumu pande zote kwa uhalifu dhidi ya binadam.