Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 10:15

Viongozi Afrika wanajadiliana mikakati ya kuimarisha uzalishaji wa chakula


Msichana mkimbizi, raia wa Somalia akitayarisha chakula nje ya hema mjini Mogadishu, Somalia Sept 20, 2016
Msichana mkimbizi, raia wa Somalia akitayarisha chakula nje ya hema mjini Mogadishu, Somalia Sept 20, 2016

Takriban Wakuu wa nchi na serikali 20 za Afrika, makampuni ya kilimo, wawekezaji wa kimataifa wanaokutana wiki hii mjini Dakar, Senegal kwa ajili ya Mkutano wa Kilele wa Chakula wa Afrika wametoa wito wa kuwepo juhudi endelevu za kukusanya rasilimali ili kufanikisha utoshelevu wa chakula barani.

Wakati wa mkutano huu wenye kaulimbiu: Lisha Afrika: Ukuu wa Chakula na Ustahimilivu, viongozi hao wanaonya kwamba theluthi moja ya watu wenye njaa duniani wako barani Afrika na kunahitajika juhudi za makusudi na endelevu katika kutumia uwezo wa Afrika wa chakula na kilimo, na utetezi wa mabadiliko kufanikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha barani.

Zaidi ya Waafrika milioni 249 wako katika hali mbaya ya ukosefu wa chakula na nchi kama Kenya zinaendelea kukabiliwa na hali mbaya zaidi ya chakula kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 40.

Marais hao pamoja na viongozi wengine wa mashirika yasiyo ya kiserikali na wanasayansi wanasema kuwa Afrika inakabiliwa na masuala ya dharura yanayozuia uendelevu wa chakula na kunahitaji kuwapo na mwelekeo wa kimakusudi wa uwekezaji wa sekta binafsi, kukabiliana na hali ya hewa na kukabiliana na athari za tabianchi, kuwekeza katika teknolojia ya kukuza vyakula mbalimbali, kuwezesha upatikanaji wa fedha, biashara na miundombinu ili kukuza sekta binafsi kupigia pondo juhudi za serikali za Afrika na kufanya maboresho ya sera ya kilimo ili kugeuza Afrika kuwa kikapu cha chakula kwa dunia nzima.

Mkutano huu wa siku tatu unaandaliwa na Macky Sall, Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, kwa ubia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, AFDB.

Wataalamu wa chakula wanasema kuwa kuongeza tija katika kilimo na uzalishaji endelevu wa chakula ni muhimu ili kusaidia kupunguza hatari ya njaa barani Afrika, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Adesina Akinwumi anasema mkutano huo unakuja wakati mwafaka na anatamani kuona Afrika ambayo inajikimu.

“Sasa ni lazima tutoke kwenye juhudi za muda mfupi hadi za muda mrefu ili kuongeza uzalishaji wetu wa chakula barani Afrika, kupunguza utapiamlo na kuhakikisha upatikanaji wa chakula barani Afrika. Ni wakati wa Afrika kulisha Afrika,” amesema Dkt Akinwumi Adesina, rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Ukosefu wa chakula kote duniani

Ulimwenguni, watu milioni 828 wanakabiliwa na njaa, huku Afrika ikiwa ni milioni 249 au theluthi moja ya idadi hiyo. Kinaya ni kwamba, Afrika pekee yenye asilimia 65 ya ardhi isiyotumika kwa kilimo ina uwezo wa kulisha watu bilioni 9 duniani ifikapo mwaka 2050. Maeneo yake makubwa ya savanna pekee yanakadiriwa kuwa hekta milioni 400, ambayo ni 10% tu ndiyo inayolimwa.

Kwa mujibu wa viongozi hao akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, William Ruto wa Kenya, Felix Tshisekedi wa DRC, Evariste Ndayishimiye wa Burundi miongoni mwa wengine wanasema, Afrika ina uwezo wa kujilisha na kuchangia kulisha dunia.

Serikali ya Kenya imeruhusu uagizaji wa tani milioni 1.5 za mahindi na mchele kutoka nje bila kulipiwa ushuru ili kukabiliana na balaa la njaa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40, kuiwezesha nchi kuwa na hifadhi ya kutosha hadi mavuno yajayo kuanzia Julai-Agosti mwaka huu. Rais William Ruto anaeleza kuwa bara la Afrika lina rasilimali za kutosha na linaweza kujikimu. Aidha, ametoa changamoto kwa viongozi wenzake wa Afrika kuangazia kilimo zaidi ya uzalishaji ili kuongeza thamani na utengenezaji. Vile vile, ametoa wito kwa vijana kuhusishwa katika juhudi za kuboresha kilimo.

"Vijana ni muhimu zaidi katika ufufuaji wa kilimo chetu. Cha muhimu zaidi, ni jinsi teknolojia inavyozidi kuongezeka, ndivyo faida inavyokuwa bora," amefafanua rais Ruto.

Vijana kuwa tegemeo katika kuzalisha chakula

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa vijana na wanawake wanastahili kuwezeshwa kuwa nguzo kuu katika ufikiaji wa utoshelevu wa chakula barani Afrika kwani ni muhimu katika sekta zote za kiuchumi kama ilivyo nchini Tanzania.

"Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii na tunatumai na tunadhani, kwa hakika, ndiyo, kwamba kwa kujenga uwezo, kwamba kwa kuweka mazingira mazuri, kwa kuweka mazingira wezeshi, vijana na wanawake, ndiyo, nchi inaweza kulisha bara zima la Afrika," anasema Samia Suluhu Hassan.

Mwishoni mwa mkutano huu wa siku tatu, ili kuhakikisha ufuatiliaji na uwajibikaji wa kutoa matokeo, mifumo ya utafiti na maendeleo, chakula cha kitaifa, na mifumo ya kilimo, marais wa bara la Afrika na viongozi wengine wanatarajiwa kuhamasisha juu dhamira ya kisiasa ya kiwango cha juu kuhusu uzalishaji, masoko na biashara, kujitolea kuhamasisha na kuoanisha rasilimali za serikali, nguvu madhubuti za washirika wa maendeleo na ufadhili wa sekta binafsi ili kufikia utoshelevu wa chakula kwa kiwango kikubwa katika kila nchi, kuendeleza miundombinu muhimu za Kilimo., kujenga na kunawiri maeneo ya usindikaji wa viwanda kujenga masoko pamoja na kuanzisha muungano wa juhudi za bara kote Afrika ili kufungua uwezo wake mkubwa wa kilimo ili kuwa kivutio cha kimataifa cha kukabiliana na uhaba wa chakula unaoongezeka duniani.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Dakar, Senegal

XS
SM
MD
LG