Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 10:25

Tanzania, Dangote zamaliza mvutano


FILE - Tajiri wa Kinigeria Aliko Dangote.
FILE - Tajiri wa Kinigeria Aliko Dangote.

Hatimaye mgogoro uliosababisha kusimamishwa kwa uzalishaji katika kiwanda cha saruji cha Dangote, kusini mwa Tanzania, inaelekea umekwisha baada ya bilionea Mnigeria Aliko Dangote na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kukutana Dar es Salaam Jumamosi.

Baada ya mkutano wao Rais Magufuli na mwekezaji huyo walitokeza mbele ya waandishi wa habari katika viwanja vya Ikulu mjini Dar es salaam na wote kuhakikisha kuwa matatizo yote yaliyosababisha kusimama kwa uzalishaji yameshughulikiwa.

Rais Magufuli na Aliko Dangote
please wait

No media source currently available

0:00 0:03:01 0:00

Rais Magufuli alisema watu aliowaita “walipiga dili” ndio walioingilia shughuli za biashara na kusababisha kukwama kwa uzalishaji. Dangote alihakikisha kuwa bado ana nia ya dhati ya kuwekeza Tanzania na kwamba anataka kununua mali zote ghafi za kiwanda hicho ndani ya Tanzania.

Mivutano kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya Dangote ilijitokeza mwanzoni mwa Disemba baada ya kampuni hiyo kutangaza inasimamisha kwa muda uzalishaji wa saruji katika kiwanda hicho kilichopo Mtwara, kusini mwa nchi hiyo.

Baada ya uamuzi huo taarifa zilizopingana zilizuka kutoka pande mbali mbali huku ikielekea kuwa serikali inalaumiwa kwa kutoipatia kampuni hiyo ushirikiano iliyoahidi tangu awali.

Kampuni ya Dangote ambayo ni mwekezaji mkubwa katika uzalishaji saruji nchini Tanzania imekuwa ikilalamika kuwa mivutano hiyo imetokana na makosa mbali mbali ambayo inadai imeletwa na watendaji wa serikali.

Mshauri wa zamani wa mawasiliano wa Dangote, Thomas Kawogo, aliyataja baadhi ya makosa hayo ni kwa serikali kushindwa kutimiza ahadi zake kwa mwekezaji huyo. Alitoa mfano kuhusu upatikanaji rahisi wa gesi kwa kampuni hiyo ambayo inategemea gesi na makaa ya mawe katika uzalishaji wa saruji.

“Sasa linapokuja suala la tunapataje gesi, tunapataje makaa ya mawe hapo ndipo pamekuwa shida”, alisema Kawogo na kuongeza ingawaje suala hilo lilishazungumziwa kati ya mwekezaji na serikali watendaji wa serikali walishindwa kutimiza ahadi zilizotolewa.

Lakini kwa upande wa serikali Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alifanunua kuhusu suala la upatikanaji wa nishati kama vile gesi na makaa ya mawe kwa kusema makaa ya mawe ambayo yamerundikana ardhini yanachimbwa pale tu mteja anapotoa maagizo ya kiwango anachokihitaji na si vinginevyo na kuongezea kuwa iwapo kuna kiwango ambacho mteja anataka basi lazima hilo lifanyike kwa kuwepo kwa mkataba, na si kinyume na hivyo.

Kuanzia awali wengi wanaohusika katika makubaliano ya serikali ya Tanzania na kampuni ya Dangote walikuwa wakilalamikia wale walioitwa “watu wa kati” kuwa ndio wanaovuruga ushirikiano wa pande hizo mbili katika kupata mali ghafi na nishati katika kiwanda hicho.

Matamshi ya Rais Magufuli Jumamosi kwamba “wapiga dili” ndio waliokuwa wakikwamisha shughuli hizo yalionyesha kuwa mawasiliano baina ya serikali na kampuni ya Dangote yalikuwa hafifu.

Tangu kuzinduliwa kwa kiwanda hicho chenye thamani ya dola za Marekani milioni 600, bei ya saruji Tanzania imeshuka kwa zaidi ya asilimia 30.

Kiwanda cha Dangote ambacho kina uwekezaji mkubwa katika saruji kuliko viwanda vingine vyote vilivyopo Afrika Mashariki kina uwezo wa kuzalisha saruji takriban tani milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1,000 mkoani Mtwara.

XS
SM
MD
LG