Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 19:10

Sudan yagubikwa na mzozo wa wakimbizi wa ndani unaoikabili dunia


FILE - Wakimbizi wa Sudan waliokimbia vita katika mkoa wa Darfur wakiwa katika kambi za muda karibu na mpaka wa Sudan na Chad huko Borota, Chad, May 13, 2023.
FILE - Wakimbizi wa Sudan waliokimbia vita katika mkoa wa Darfur wakiwa katika kambi za muda karibu na mpaka wa Sudan na Chad huko Borota, Chad, May 13, 2023.

Taifa la Sudan barani Afrika limegubikwa na  mzozo mkubwa sana wa wakimbizi wa ndani duniani.

Takriban watu milioni 5.6 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan baada ya mapigano ya zaidi ya miezi sita, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu.

Watalam wa masuala ya kutetea haki za binadamu wanahofia kuwa nchi hiyo huenda ikatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Jinsi Vita Ilivyoanza

Kilichoanza kama mapigano nchini Sudan Aprili mwaka 2023 kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na kikosi cha RSF, huenda kikaitumbukiza Sudan katika 'vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Miezi sita ya mzozo huo, imesababisha mamilioni ya watu kuhama makwao. Twakimu kutoka shirika La Kimataifa la Uhamiaji, IOM, zinaeleza kuwa watu milioni 7.1 wamehama makwao ndani ya nchi hiyo.

Hata hivyo hali ya Sudan haivutii hisia za kidiplomasia wala kisiasa. Profesa Macharia Munene anasema mgogoro wa hivi punde wa Mashariki ya Kati huenda unachangia kwa mzozo wa Sudan kusahaulika.

Profesa Macharia aeleza mzozo haupungui

Profesa Munene Macharia- Mchambuzi masuala ya Diplomasia-Kenya anaeleza: “Huo mzozo haupungui unazidi, vile imefanyika ni Darubini za Dunia zimeondoka Sudan na kwenda sehemu nyingine kama vile huko Gaza, kwa hiyo sio watu ambao wanaangazia hapo kwa sababu kuna tatizo jingine ambalo linavutia watu zaidi lakini vita vinaendelea na watu wanaendelea kuumia”

Marekani na Saudi Arabia zimehimiza usitishaji wa mapigano mara kadhaa kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha RSF katika mazungumzo ya Jeddah tangu Mei, lakini mapigano yameendelea Khartoum na kwingineko, huku kila upande ukiushutumu upande mwingine.

Juhudi za Saudi Arabia Kuleta Amani

Kumekuwa na juhudi nyingi za kuleta amani ambazo zimeonakana kugonga mwamba hata hivyo mazungumzo kati ya pande zinazopigana nchini Sudan yanatarajiwa kuanza tena hivi leo mjini Jeddah, Saudi Arabia, yakilenga kupata suluhu na vilevile jinsi ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia .Taswira ya Sudan imekuwa ya kusikitisha huku raia wakihisi kusahaulika. Abdullahi Boru ni mtaalam wa masuala ya wakimbizi, Marekani anaeleza:

“ Kulikuwa na ule mchakato wa Jeddah nchini Saudi Arabia na haujaleta matumaini kwa watu kwa kuwa wale ambao walipigania kumuondoa rais wa Zamani Omar Al-Bashir walihisi hawajahusishwa, kando na hayo makundi yote mawili hayahisi kama mchakato huu utaweza kuleta amani, kwa hiyo hawajakubaliana kama ilivyohitajika.”

Sudan iliyogawanyika

Khartoum, iliyowahi kuwa Taswira kuu ya Sudan iliyoungana, iliyo na uhuru, sasa iko mikononi mwa RSF, isipokuwa baadhi ya ngome za SAF. Hatima ya jiji hilo litategemea kama SAF itapeleka silaha au nguvu za anga kuwaondoa RSF, cha kusikitisha ikiwa ni kwa gharama kubwa ya maisha ya binadamu na nyenzo.

Boru anaongeza kuwa: “Kwa sababu ya vita hasa maeneo ya Darfur magharibi mwa nchi hiyo pamoja na Khartoum, maeneo ambayo kwa kweli mashirika ya kutoa misadaa hayawezi kuingia kwa sababu ya vita ,kwa hiyo pasi na kuwepo usitishwaji wa mapigano itakuwa vigumu sana kwa watu hao ambao wanahitaji vyakula na msaada kuweza kusaidiwa.”

Vita hivi aidha vimeharibu sekta ya kilimo nchini Sudan, vimewatumbukiza watu zaidi ya milioni 4 katika janga la wakimbizi wa ndani, zaidi ya milioni 1 wakimbizi walio nje ya mipaka ya Sudan, na ukosefu wa usalama. Mikoa mitatu inayokumbwa na uhaba wa chakula ikiwa ni Khartoum, Darfur, na Kordofan, maeneo yote yakiwa na mzozo mkubwa zaidi.

Mtaalam wa Masuala ya Diplomasia

Macharia Munene-Mtaalam wa masuala ya Diplomasia-Kenya anasema:“Nchi kama Chad inataabika , na Chad yenyewe ni nchi maskini na sasa imeongezewa mzigo ambao hawajui watafanya nini , lakini misaada ambayo inafaa ipelekwe Chad maana watu wengi wametorokea huko.”

Lakini Je vita vya Sudan vimekuwa na athari gani kwa kanda?

Munene anasema kuwa: “Hii kanda yote shida yake imeongezeka kwa sababu ya mzozo wa Sudan ,tusipo taja wengine , kwahiyo ukilinganisha hizo zote hakuna maendeleo ni kurudi nyuma.”

Kwa upande wake Boru anaeleza: Imeathiri Kanda nzima , ukikumbuka kabla ya mapigano nchi ya Sudan ilikuwa imewapa hifadhi wakimbizi Millioni 1.1 wengi wao wakiwa raia kutoka sudan kusini…… kwa sababu ya vita katika eneo la Darfur wengi wa watu hao wanaelekea Chad ,nchi ambayo ukiangalia hali ya kiuchumi,hali ya siasa , nchini yenyewe inamatatizo chungu nzima. Kwa hivo kuwepo kwa vita hivi au kuendelea imefanya kanda nzima kuathirika”

Wakati vita vikiendelea Sudan , wahusika mbalimbali wanalazimika kuunda ushirikiano na pande zinazopigana au kuchukua hatua za kulinda uwepo wao nchini Sudan.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Hubbah Abdi, Washington, DC.

Forum

XS
SM
MD
LG