Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 12:25

Mwandishi wa kike auwawa mjini Mogadishu


Waandishi katika kituo cha radio cha Shabelle wakijadili mashambulizi yanayowalenga waandishi wa Somalia, mjini Mogadishu.
Waandishi katika kituo cha radio cha Shabelle wakijadili mashambulizi yanayowalenga waandishi wa Somalia, mjini Mogadishu.

Mwandishi wa habari wa kike nchini Somalia, Sagal Salad Osman aliyekuwa akifanya kazi kwenye radio na televisheni ya seriakli amepigwa risasi na kuuawa mjini Mogadishu siku ya Jumapili.

Mohammed Ibrahim Moalimuu, katibu mkuu wa chama cha kitaifa cha waandishi wa habari nchini Somalia, ameiambia VOA kwamba Sagal Osman alipigwa risasi ya watu wasiojulikana katika wilaya ya Hodan wakati akiondoka kwenye eneo la chuo kikuu. Amesema watu waliokuwa na silaha walikimbia haraka kutoka kwenye eneo la tukio.

"Tunaalani vikali, na tunaitaka serikali kuchunguza na kuwafikisha mbele ya sheria wale waliohusika na mauaji hayo," amesema.

Abdirahman Yusuf al-Adaala, mkurugenzi wa shirika la habari la Somalia, amesema Sagal Osman ambaye alikuwa katika umri wa miaka ya mwanzo ya 20 alikuwa mzalishaji na mtangazaji wa vipindi vinavyohusu masuala ya vijana.

Sagal Osman ni mwanamke wa pili mwandishi wa habari kuuawa nchini Somalia katika muda wa miezi sita iliyopita.

Desemba mwaka jana, Hinda Haji Mohammed, mwandishi wa habari mwanamke ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye shirika la habari la serikali, aliuawa na bomu la kwenye gari mjini Mogadishu. Kundi la kigaidi la al shabaab lilidai kuhusika na shambulizi.

Somalia ni moja ya nchi hatari sana duniani kwa wafanyakazi wa kwenye vyombo vya habari.

XS
SM
MD
LG