Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 07:42

Dr. William Samoei Ruto: muuza kuku ambaye sasa ni rais wa Kenya


Rais wa Kenya Dr. William Ruto Septemba 5, 2022. Picha: Reuters
Rais wa Kenya Dr. William Ruto Septemba 5, 2022. Picha: Reuters

Dr. William Samoei Ruto, rais wa Jamhuri ya Kenya. Ni mtu mwenye historia ndefu lakini iliyopatikana kwa haraka ndani ya miaka 55 ya maisha yake; mchanganyiko wa maisha magumu na ufanisi mkubwa maishani.

Ruto ameweka historia kwa kuwa mgombea wa kwanza wa urais katika Jamhuri ya Kenya kushinda kura za urais katika jaribio la kwanza.

Amekuwa naibu wa kwanza wa rais kushinda kiti cha urais katika Jamhuri ya Kenya.

Mwanasiasa ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote. Mwanasiasa ambaye ametajwa na wachambuzi kama mchapa kazi na mwenye bidii na kiu ya kupata kile anacholenga maishani. Mtu asiyekata tamaa.

Mcheshi katika hotuba zake, anayesemekana kutaka kujua kila linaloendelea karibu naye, mtu mkarimu mwenye roho ya kuchangisha pesa kwa watu na kwa ajili ya miradi mbalimbali.

Ruto ameshutumiwa kwa kashfa kadhaa hasa za ufisadi bila kesi kufikishwa mahakamani, na ameshinda karibu kesi zote ambazo zimewahi kufunguliwa mahakamani dhidi yake ikiwemo kesi katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

Yafuatayo ndiyo mambo muhimu yanayomhusu rais wa 5 wa Jamhuri ya Kenya Dr. William Samoei Ruto.

Majina Kamili: William Samoei Arap Ruto

Umri: miaka 55

Mke wake: Rachel Chebet Ruto

Watoto: sita

Baba: Daniel Cheruiyot

Mama: Sarah Cheruiyot

Maisha ya utotoni na masomo

William Samoei Ruto alizaliwa Desemba 21 1966 katika kijiji cha Kamagut, kaunti ya Uasin Gishu, nchini Kenya.

Alizaliwa katika familia maskini ambayo haikuweza hata kumnunulia viatu. Alikuwa akitembea bila ya viatu hadi alipofikisha umri wa miaka 15, alipokuwa anajiunga na shule ya upili ndipo akavaa viatu.

Alianzia masomo katika shule ya msingi ya Kamagut, na katika shule ya upili ya Wareng, iliyoko Eldoret kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.

Amekuwa akisema kwamba wakati anasoma, alikuwa akiuza kuku na karanga barabarani kwa wasafiri ili kupata karo. Kuna picha za utotoni zinazoonyesha hilo. Hata akiwa naibu rais amekuwa akiongoza wachuuzi na wanunuzi katika masoko ya kuuza kuku.

Alijiunga katika shule ya upili ya Kapsabet, kaunti ya Nandi kwa masomo ya kidato cha 5 na 6.

Alifundisha katika shule kadhaa za upili, katika sehemu za Sugoi na Kamagut.

Baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi kwa masomo ya shahada katika sayansi ya mimea na wanyama. Alipata shahada yake mwaka 1990, akiwa wa kwanza katika darasa lake.

Kutokana na kuwa mshindi katika darasa lake, chuo kikuu cha Nairobi kilimpa ufadhili wa kusoma shahada ya uzamili.

Alianza masomo ya shahada ya uzamili mwaka 1991 lakini akasitisha baadaye alipoanza siasa. Alirudi darasani baadaye na kumaliza masomo ya shahada ya uzamili mwaka 2011. Alisajiliwa tena katika chuo hicho cha Nairobi na kukamilisha masomo mwaka 2018 akiwa na shahada ya juu ya udaktari yaani Phd.

Siasa

Safari ya Dr. William Ruto kisiasa ilianza mwaka 1992 akiwa katika chuo kikuu cha Nairobi.

Aliwahi kufanya kazi na Prof Julia Ojiambo, mmoja wa wanawake wakongwe katika siasa za Kenya.

Pamoja na vijana wenzake katika chuo kikuu cha Nairobi, akiwemo Cyrus Jirongo na Kipruto Kirwa, waliunda chama cha United Democratic Movement UDM, lakini akakikimbia na kujiunga rasmi na chama kilichokuwa madarakani wakati huo, Kenya National African Union KANU, chini ya utawala wa aliyekuwa rais wa Kenya Hayati Daniel Toroitich Arap Moi.

Moi aliwakusanya vijana shupavu wa chuo kikuu cha Nairobi ili kukipa umaarufu chama kilichokuwa madarakani cha KANU, kwa matayarisho ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Vijana hao, akiwemo William Ruto na Cyrus Jirongo walifahamika kama kundi la vijana wa Kanu – YK’92. Moi alikuwa anakabiliwa na ushindani mkali sana baada ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Vijana wa YK’92, walipewa pesa kuwashawishi wapiga kura ili kukabiliana na wimbi kali la upinzani ambalo lilikuwa linatishia utawala wa rais Daniel Toroitich Arap Moi.

Vijana wa Kanu, YK’92, waliwaahidi vijana nafasi za kazi na kuahidi kuinua maisha ya watu mashinani hasa jamii ndogo ndogo, na Ruto alikuwa mstari wa mbele kufanikisha ajenda hiyo ya Moi.

Ruto na vijana wenzake walifuata maagizo ya Moi, wakatoa pesa kwa wapiga kura hasa sehemu ambazo upinzani ulikuwa umepata uungwaji mkono mkubwa, na kuwahadaa baadhi ya wanasiasa wa upinzani kujiunga na chama kinachotawala. Upinzani ulipoteza watu maarufu waliokimbia na kujiunga na Moi.

Wakati huo, Ruto alikuwa na umri wa miaka 25. Kando na kupewa pesa na rais Moi kumaliza nguvu ya upinzani, alikuwa anapewa mafunzo ya kisiasa na Moi namna ya kukabiliana na upinzani.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, Kenya ilikuwa inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi baada ya kunyimwa misaada kutokana na rekodi mbaya ya haki za kibinadamu na dhuluma dhidi ya upinzani.

Nchi pia ilikuwa inakabiliwa na visa vya ufisadi vilivyokithiri, maandamano, dhuluma za polisi na hali tete ya kisiasa.

Ruto kujiingiza katika siasa.

Miaka mitano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, William Ruto aliamua kujiingiza kabisa katika siasa na kushinda kiti cha ubunge cha Eldoret Kaskazini mwaka 1997. Alimshinda mwanasiasa maarufu sana nchini kenya wakati huo Reuben Kiplagat Chesire.

Kwa kumshinda Chesire, Ruto alijulikana Kenya mzima. Kabla ya kuingia siasa, Chesire alikuwa mkuu wa wilaya, mwafrika wa kwanza kuwakilisha muungano wa wakulima Kenya, na mwenyekiti wa wamiliki hoteli na muungano wa wafanyabiashara wa utalii Afrika.

Ruto alikuwa mbunge wa Eldoret Kaskazini tangu mwaka 1997 hadi 2007 kwa tiketi ya chama cha KANU na baadaye kutetea nafasi hiyo kwa tiketi ya chama cha Orange Democratic Movement ODM, katika uchaguzi wa mwaka 2007 na 2013.

Moi alimteua Ruto kuwa waziri msaidizi katika ofisi ya rais, nafasi ambayo aliishikilia kati ya mwaka 1998 hadi 2002. Baadaye alimteua kuwa waziri wa mambo ya ndani, kati ya mwezi Agosti hadi Desemba 2002, muda mfupi kabla ya Moi kustaafu.

Ruto alikuwa upande wa upinzani na Uhuru Kenyatta baada ya KANU kushindwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2002. Alikosoa sana namna utawala wa Mwai Kibaki ulivyokuwa unazungumzia utawala wa rais mstaafu Daniel Moi.

Ruto alikuwa katibu mkuu wa chama cha Kenya African National Union KANU, mwaka 2005, ambapo alisimamia shughuli na mipango ya chama hicho.

Kuvunjika kwa urafiki kati ya Odinga na Kibaki, kuanza kwa urafiki kati ya Ruto na Odinga

Kundi la wanasiasa ambalo lilionyesha kutofurahia utawala wa Mwai Kibaki likiongozwa na Raila Odinga, liliondoka katika muungano wa Rainbow.

Miongoni mwa wanasiasa hao walikuwa kutoka chama cha Liberal Democratic LDP, cha Odinga. Wengine walikuwa Kalonzo Musyoka, Prof Anyang’ Nyong’o, Ochillo Ayacko, William ole Ntimama, Najib Balala na Linah Kilimo.

Baadhi yao walikuwa mawaziri kabla ya kufutwa kazi na Kibaki kwa kukataa kuunga mkono rasimu ya katiba ya mwaka 2005.

Walianzisha upinzani dhidi ya serikali waliyokuwa wameunda, kwa kuunda chama cha Orange Democratic Movement, ODM. Waliungana na Uhuru Kenya na wanasiasa wengine wa chama cha Kanu Akiwemo William Ruto ambao pia walikuwa wanapinga rasimu hiyo ya katiba.

Ruto alitumia fursa hiyo kushawishi wanasiasa kutoka bonde la ufa kama Henry Kosgey kujiunga na chama cha ODM na kuhama Kanu.

Chama cha ODM pia kilivunjika na kuunda ODM - Kenya, baada ya wanasiasa waliokuwa wanamtaka Kalonzo Musyoka kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2007 kuona kwamba Raila hakuwa tayari kutoa nafasi hiyo kwa Musyoka kugombea urais.

Ruto alibaki na Odinga na kumuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Uhuru Kenyatta, na chama chake cha KANU alikimbia ODM na kumuunga mkono Mwai Kibaki.

Kiu cha Ruto cha kugombea urais kilianza mwaka miaka michache baada ya Moi kustaafu

Kabla ya Uhuru kuondoka ODM, Ruto alikuwa tayari ametangaza kwamba naye alikuwa anataka tiketi ya chama cha KANU kumenyana na Odinga, Musyoka ndani ya ODM. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa kifo rasmi cha chama cha KANU.

Wakati KANU kinashirikiana na ODM, Ruto akiwa katibu mkuu wa chama cha KANU, alitangaza kugombea urais. Tangazo lake lilikuwa limetolewa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Hatua hiyo hata hivyo haikupokelewa vyema na vigogo wa chama chake cha KANU. Alijiuzulu nafasi ya katibu mkuu wa KANU na kuhamia chama cha Orange Democratic Movement chake Raila Odinga, akitaka kuungwa mkono na Odinga, kugombea urais katika uchaguzi ambao tayari ulionekana kuwa na ushindani mkali kati ya Odinga na Mwai Kibaki.

Chama cha ODM kilikataa kumpa tiketi William Ruto na badala yake kumpa Raila Odinga.

Ruto alibaki katika ODM na kumuunga mkono Raila Odinga, baada ya kuahidiwa kuwa waziri mkuu endapo Odinga angeunda serikali.

Alimfanyia kampeni Odinga na kushinda kura za Rift Valley ambako chama cha KANU kilikuwa na ufuasi wa muda mrefu.

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 yalikumbwa na utata baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Mwai Kibaki mshindi. Odinga, Ruto na wanasiasa wengine wakiwemo Musalia Mudavadi, waliyakataa matokeo hayo.

Ghasia zilitokea, maelfu ya watu wakafariki, watu wakajeruhiwa na mali kuharibiwa.

Kibaki na Odinga walikubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Odinga akawa waziri mkuu. William Ruto aliteuliwa waziri wa kilimo na baadaye akahamishwa na kuwa waziri wa elimu ya juu.

Odinga akiwa waziri mkuu, alitangaza kwamba alikuwa amemsimamisha kazi William Ruto kwa shutuma za ufisadi.

Ilidaiwa kwamba Ruto alikuwa ameuza mahindi ya serikali na kuweka pesa mfukoni, madai ambayo anakana hadi sasa. Hakuna ushahidi uliotolewa wala kushitakiwa mahakamani.

Ruto alikataa kuondoka madarakani na kusema kwamba aliyemteua alikuwa Mwai Kibaki na wala sio Raila Odinga.

Mwai Kibaki alikataa kutekeleza tangazo la Odinga, na badala yake akamtoa Ruto kutoka wizara ya kilimo hadi ya elimu ya juu.

Hapo ndipo uhasama mkali wa kisiasa kati ya William Ruto na Raila Odinga ulidhihirika, na hapo ndipo upinzani mkali wa kisiasa ulianza baina yao.

Ruto aliondoka chama cha ODM na kuunda chama chake cha United Republican Party URP, Januari 15, 2012.

Mashtaka ya uhalifu ICC

Mwaka 2011, William Ruto, pamoja na watu wengine sita akiwemo Uhuru Kenyatta, walifunguliwa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.

Walishtakiwa kwa shutuma za kuchangia pakubwa katika machafuko yaliyoua watu 1,200, kusababisha uharibifu wa mali katika uchaguzi wa mwaka 2007/2008.

Kesi hiyo ilitupiliwa mbali mwaka 2016 kwa kukosekana ushahidi, japo kuna ripoti kwamba mashahidi walihongwa au walitishwa.

Kuna ripoti pia kwamba kesi hiyo iliingiliwa kisiasa na kwamba Raila Odinga alikuwa miongoni mwa wanasiasa maarufu waliotaka Ruto na Kenyatta wafungwe jela ili asiwe na ushindani katika uchaguzi wa mwaka 2013. Raila amekana madai hayo kila mara.

Muungano wa mawakili kuomuoredhesha Ruto kati ya mafisadi wakubwa Kenya

Muungano wa mawakili nchini Kenya ulichukua hatua ya kuorodesha kile kilitajwa kama majina ya watu fisadi zaidi nchini kenya, mwaka 2012.

Miongoni mwa majina hayo lilikuwemo la William Samoei Ruto.

Orodha hiyo hata hivyo ilisemekana kwamba ilikuwa imechochewa kisiasa. Muungano wa mawakili ulitaka wapiga kura kutowapigia kura watu walioorodheshwa.

Licha ya orodha hiyo, Ruto na chama chake cha URP, alijiunga na Uhuru Kenyatta, ambaye pia alikuwa amehama chama cha KANU na kuunda The National Alliance TNA, na kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, na kuwa naibu wa rais. Vyama vyao viliungana na kuunda muungano wa Jubilee, wakati Kenya ilikuwa inasherehekea miaka 50 ya uhuru.

Walimshinda Raila Odinga na muungano wake wa Coalition for Reforms and Democracy CORD, akiwa pamoja na Kalonzo Musyoka, Moses Wetangula, Musalia Mudavadi, miongoni mwa wengine.

Ruto aliongoza juhudi za kuvunja vyama tanzu kadhaa vilivyounda muungano wa Jubilee, na kuunda chama cha Jubilee ambacho kilishinda marudio ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 baada ya kufutiliwa mbali na mahakama.

Odinga alisusia marudio ya uchaguzi huo na badala yake kujiapisha kama rais wa wananchi na kuitisha maandamano.

Ushirikiano wa Kenyatta na Odinga wamtema Ruto

Rais Uhuru Kenyatta aliamua kuanza ushirikiano na Raila Odinga hatua ambayo ilipelekea uhusiano wake na William Ruto kuvunjika.

Ruto na wanasiasa walio karibu naye waliripoti kutengwa na serikali na majukumu yao kupewa watu wengine.

Chama cha Jubilee kilikumbwa na migogoro.

Ruto alihama Jubilee na kuunda chama chake cha United Democratic Alliance UDA, Januari 2021.

Wanasiasa kadhaa walihama Jubilee na kujiunga na UDA, huku uongozi wa Jubilee ukiwaadhibu.

Wachambuzi wa siasa za Kenya wanasema kwamba kampeni ya Ruto ambayo imepelekea kushinda urais, imekuwa na mtindo sawa na aliotumia aliyekuwa rais wa pili Hayati Daniel Toroitich Arap Moi, mwaka 1992 wakati Ruto alikuwa katika kundi la YK’92.

Ruto hajawahi kushindwa katika kila analofanya kati ya yale yanayojulikana.

Tangu alipozaliwa, historia inaonyesha kwamba Dr. William Ruto amekuwa akifanikiwa katika kila hatua anayofanya. Wanaomjua kijijini alikozaliwa wameviambia vyombo vya habari vya Kenya kwamba alikuwa muuzaji mzuri sana wa kuku na karanga ambaye alipata faida.

Shuleni, alifanikiwa katika masomo. Alikuwa wa kwanza alipokuwa anasoma shahada zake ikiwemo PHD.

Ameshinda viti vyote vya kisiasa ambavyo amegombea.

Amewaangusha vigogo wa kisiasa tangu mwaka 1997 akiwemo Reuben Kiplagat Chesire ambaye alikuwa mwanasiasa aliyeogopewa sana Eldoret.

Amemshinda rais Uhuru Kenyatta na mwanasiasa mwenye sifa kubwa kote Afrika mashariki na ambaye amekuwa katika siasa za Kenya kwa muda mrefu Raila Odinga wakiwa wameungana.

Hajawahi kupoteza kesi mahakamani isipokuwa kesi ya ardhi ambapo alisema aliyekuwa amemuuzia alimhadaa.

Alikuwa amekata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama lakini akaamua kuondoa rufaa hiyo na kuachana na ardhi hiyo.

Ni mwanasiasa wa kwanza kugombea urais wa Kenya na kushinda kwa mara ya kwanza. Pia, ni naibu rais wa kwanza wa Kenya kugombea urais na kushinda.

Ushindi wa jasho, ushindi wa mahangaiko

Wachambuzi wa siasa nchini Kenya wamekuwa wakisema kwamba ushindi wa Dr. William Ruto alikuja kwa ‘mahangaiko’ kutoka kila sehemu yakiongozwa na serikali aliyokuwa akitumikia kama naibu rais.

Vyombo vya habari vya Kenya, sawa na mashirika ya kukusanya maoni, vilikuwa vimetabiri kwamba Ruto angeshindwa na Raila Odinga.

Kuna wakati Dr. Ruto aliambiwa atoke kwenye makazi ya naibu rais kwa sababu nyumba hiyo ambayo inamilikiwa na serikali, ilikuwa imepangiwa kupakwa rangi.

Kampeni zikielekea kumalizika, Ruto alisikika akimkosoa rais Uhuru Kenyatta kwa kumhangaisha.

“Nataka nimuombe rais wetu wa Kenya, tafadhali bwana rais, hustahili kuwa chanzo cha vitisho nchini Kenya. Wacha kutisha wakenya. Kazi yako ni kuhakikisha kwamba wakenya wote wako salama. Wacha kutuambia ya kwamba tutakujua kwamba wewe ni rais. Sisi ndio tulikuchagua uwe rais wa Kenya. Wacha kututisha. Wacha kuniletea maneno rafiki yangu. Wewe sukuma mgombea wako bwana kitendawili (Raila Odinga). Unaniongelea nini? Rais, tafadhali, wacha kuzungumza kunihusu. Zungumzia mgombea unayempendelea….. tuambie ajenda ya huyo jamaa (Raila Odinga) achana na William Ruto. Nilikuunga mkono wakati ulitaka mtu wa kukuunga mkono. Kama hutaki kuniunga mkono, achana na mimi kabisa. Kwa heshima, tafadhali rais, kuwa mungwana. Kuwa na shukrani. Wewe sasa umeanza kunitisha? Bora usiuwe watoto wangu. Lakini mimi na wewe tafadhali tuheshimiane”, alisema Ruto katika mkutano wa kisiasa mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi, kusini magharibi mwa Eldoret, Kenya, uliokuwa umejaa wafuasi wake na kuonyeshwa moja kwa moja na televisheni za kenya pamoja na mitandao ya kijamii.

Kipawa cha kuunda marafiki

Licha ya kujibizana vikali na rais Uhuru Kenyatta katika muda wa miaka 4 iliyopita, Dr. Ruto amesema kwamba hana kinyongo na mtu yeyote na kwamba kila mtu ni rafiki yake na yupo tayari kufanya kazi na mtu yeyote.

Amesema hana kinyongo na Kenyatta kwamba alikataa kumuunga mkono licha yake kumuunga mkono mwaka 2012 na 2017.

Wengi wa wanasiasa wanaomzunguka Ruto, walikuwa wapinzani wake na ambao walikuwa wafuasi na wanasiasa wa karibu sana na Raila Odinga.

Miongoni mwao ni Moses Wetangula ambaye sasa ni spika wa bunge la taifa, Amason Kingi ambaye sasa ni spika wa baraza la senate, Musalia Mudavadi ambaye alikuwa msitari wa mbele katika kumtafutia kura Raila Odinga mwaka 2017, miongoni mwa wengine wengi.

XS
SM
MD
LG