Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 06:18

Kaimu Rais wa Nigeria ajadili ghasia za kidini


Kaimu Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amekutana na wakuu wa usalama huko Abuja, wakati maafisa wa mji wa kati wa Jos na wakazi wa vijiji wakiwa wanawazika katika makaburi ya pamoja, mamia ya waathiriwa wa ghasia za mwishoni mwa wiki, wengi wao wanawake na watoto.

Msemaji wa serikali ya jimbo, Gregory Nianlong amesema kiasi ya watu 500 walichinjwa wakati wa shambulio la usiku dhidi ya vijiji vitatu karibu na Jos, mji mkuu wa Jimbo la Plateau. Hakuna habari huru kuthibitisha idadi hiyo. Waathiriwa wengine wanatibiwa huku watuhumiwa 100 wamekamatwa.

Vikosi vya usalama vimeamrishwa kuwasaka walohusika na mashambulio hayo. Mchambuzi wa kisiasa huko mjini Lagos, George Eke ameiambia Sauti ya Amerika kwamba ukosefu wa nafasi za ajira na ufukara uliokithiri ni mambo yanayochochea hali hii ya ghasia iliyotokea huko Jos.

"Sehemu kubwa ya matatizo haya yanasababishwa na wanasiasa. Nigeria imetajwa hasa upande wa kaskazini kuwa eneo ambalo Al-Qaida inaweza kuwa na ushawishi, na kuwaandikisha watu kwa shughuli zake."

Mapambano kati ya makabila yenye uhasama na makundi ya kidini yalisababisha mauwaji ya watu 320 mwezi Januari huko Jos kufuatana na polisi. Wanaharakati wa kidini na haki za binadam wanasema idadi jumla ya ghasia hizo ilifikia 500. Ghasia za wiki hii zilikua kati ya wafugaji wa kiislamu na wanavijiji wa kikristo.

XS
SM
MD
LG