Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 08:02

DRC yajiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki


Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakishiriki mkutano kwa njia ya video.
Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakishiriki mkutano kwa njia ya video.

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumanne waliidhinisha na kuikaribisha  rasmi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwenye uanachama mpya wa jumuiya hiyo inayokuwa na wanachama saba sasa.

Hii ni kufuatia mapendekezo ya kikao cha baraza la mawaziri cha tarehe 25 Machi kwamba Congo imekidhi vigezo vya kujiunga na jumuiya hiyo kongwe barani Afrika baada ya mchakato mrefu.

"Waheshimiwa maraisi ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana kwa kunikaribisha katika mkutano huu maalumu ambapo kwa mara ya kwanza ninazungumza kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kama mwanachama mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema rais Tshisekedi.

Hali kadhalika rais huyo alisema anatarajia kwamba kuwa ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutaisaidia nchi yake kuwa na ulinzi na usalama hasa eneo la Mashariki mwa Congo ambalo linakumbwa na machafuko.

DRC, yenye takriban raia milioni 90 ni taifa la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Algeria iliyoko kaskazini mwa Afrika.

Katika kikao cha Jumanne Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye ndiye menekiti wa sasa wa Jumuiya hiyo, alisema DRC Kujiunga na Jumuiya hiyo ni "jambo la kihistoria."

Naye Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema anatumai kwamba wananchi wa DRC na wa nchi zingine wanachama watafaidika na hatua hiyo.

"Tanzania inasema karibu sana DRC. Ni matumaini yangu kwamba DRC inauharakisha mchakato wa kukamilisha makubaliano yaliyo katika mkataba wa kujiunga, ili kuwapa wananchi wake fursa ya kufurahia matunda ya jumuiya. Maamuzi yenu ya kujiunga na jumuiya yatasaidia kupatikana na amani na ulinzi, umoja na mshikamano sio tu Congo bali kwa jumuiya nzima kwa ujumla.”

Wachambuzi wanasema DRC kujiunga na EAC kuna mafanikio chung nzima kwa wadau wote kwani inatengeneza wigo mpana zaidi wa kibiashara kuanzia bahari ya hindi mpaka ya atlantiki.

"Ni hatua ya kushabikiwa na nchi zote wanachama kwa sababu ya manufaa yake hususa katika nynja ya kiuchumi," Dk Bravious Kahioza, mtaalam wa masuala ya Uuchumi kutoka Dar es Salaam, Tanzania, aliiambia Sauty ya Amerika kwa njia ya simu.

Naye katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki ansema mafanikio makubwa zaidi yatapatikana pale vikwazo vyote vya kibiashara baina ya nchi wanachama vitaondolewa.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilianzishwa mwaka wa 2000 baada ya ile ya awali kusambaratika mnamo mika ya 70, inaundwa na na nchi saba ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi,Sudan Kusinina Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ambayo imekuwa mwanachama rasmi kuanzia leo.

XS
SM
MD
LG