Kiongozi huyo wa Ukraine anafanya ziara katika nchi tatu akitafuta msaada kutoka kwa washirika wake wa Ulaya, wakati vita vya Russia nchini Ukraine vikielekea kumaliza mwaka mmoja.
Maafisa wa Ukraine wamesema wanatarajia Russia kuimarisha mashambulizi katika sehemu za mashariki mnamo Februari 24 wakati vita hivyo vikitimiza mwaka.
Akihutubia bunge la Uingereza, Zelenskyy ametaka kupewa ndege za kivita ili kuimarisha mashambulizi na kuhakikisha ushindi dhidi ya Russia.
Ziara yake nchini Uingereza imefanyika wakati Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ametangaza kuwa Uingereza itatoa mafunzo kwa marubani wa Ukraine namna ya kutumia ndege za kivita zilizoidhinishwa na muungano wa NATO.
Zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Ukraine wamepokea mafunzo nchini Uingereza ya utumiaji vifaru ambavyo Uingereza imevitoa kwa Ukraine.
Lavrov yupo Sudan siku mbili baada ya wanadiplomasia wa Marekani kumaliza mazungumzo
Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov anatarajiwa Khartoum, Sudan, ambapo atakutana na viongozi wa kijeshi na kujadiliana kuhusu uhusiano wa Sudan na Russia, pamoja na mambo mengine.
Kulingana na shirika la habari la serikali ya Sudan, SUNA, mazungumzo kati ya Lavrov na viongozi hao wa kijeshi pia yataangazia mchango wa Khartoum katika kumaliza mgogoro wa usalama katika nchi Jirani zikiwemo Chad, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Afrika ya kati.
Ziara ya Lavrov nchini Sudan inajiri wakati wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka Marekani na nchi zingine za ulaya, wamemaliza mazungumzo ya siku mbili na viongozi wa kijeshi wa Sudan na watetezi wa demokrasia.
Mazungumzo hayo yalilenga kuhakikisha kwamba makubaliano yanapatikana kuhusu uundwaji wa serikali ya Umoja wa kitaifa na kuimarisha demokrasia nchini Sudan.
Mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021, yalipelekea kuvunjika kwa utawala wa mpito uliokuwa umehudumu kwa muda mfupi, baada ya kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir katika mapinduzi ya April 2019 kufuatia maandamano ya kiraia.
Lavrov ametembelea nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Mali na Mauritania.
Hii ni mara ya pili mwanadiolomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia kutembelea Afrika, akilenga kuimarisha maslahi ya Russia barani Afrika.