Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 23, 2024 Local time: 03:23

Zambia: Mafuriko mabaya kuwahi kutokea yameathiri zaidi ya watu 400,000


Ramani ya Zambia
Ramani ya Zambia

Maafisa nchini Zambia wanasema mwaka huu takriban watu 400,000 wameachwa bila ya makazi kutokana na mafuriko mabaya sana kuwahi kutokea katika nusu karne – ambayo yalianza kiasi cha wiki nne zilizopita.

Mvua kubwa sana zilianza mwezi mmoja uliopita na kusababisha kingo za mito kufurika, mafuriko yamezikumba maelfu ya nyumba na watu kulazimika kuhamia katika makazi ya muda.

Wakati baadhi ya watu mjini Lusaka, wameondoka kwenye nyumba ambazo zimeharibiwa na mafuriko mabaya sana ambayo yalianza kiasi cha wiki nne zilizopita, wengine akiwemo Joan Chikwa, yeye hajaondoka. Anaishi katika nyumba na wanafamilia 19. Anasema hawana fedha kuangalia makazi mbadala.

“Kama ukiangalia, utaona kwamba wale wenye fedha wamehama na wamefanikiwa kuhamia kwingineko. Ndiyo maana sisi umetukuta hapa. Choo hakifanyi kazi kwasababu ya mvua. Watoto wetu hawaendi shule, isipokuwa watu wazima. Lazima tuwabebe kwenye migongo yetu kuwavusha. Waume zetu hawana kazi, kwasababu kule ambao walikuwa wanafanyia kazi kumejaa maji. Kwahiyo tunauliza kama kuna aina yoyote ya msaada,” anasema Chikwa.

Hilo linamtia wasi wasi Mainda Simataa, afisa manispaa wa Lusaka, hata kliniki zimefungwa. “Tuna baadhi ya watu ambao chakula na mali zao zimeoshwa na mafuriko, na hawana chochote cha kuishi nacho kwa wakati huu. Kwangu mimi, shinikizo ni kuhakikisha kwamba familia kama hizo zinasaidiwa haraka iwezekanavyo,” ameongezea Simataa.

Busiku Sulwe, rais wa Taasisi ya Mipango Zambia anasema Lusaka imejengwa kwenye mawe, kwahiyo mfumo wa maji taka ni wa pole pole sana, na hivyo husababisha mafuriko. Amependekeza kwamba mji ufanyie ukarabati mfumo wa maji taka ili kuzuia mafuriko wakati kuna mvua nyingi, kama ilivyokuwa katika msimu wa mwaka 2022 na 2023.

Sulwe anasema “Pia tumahitaji kuangalia katika kuimarisha kazi ya udhibiti wa maendeleo katika mamlaka za kieneo ili tuweze kuzuia maendeleo ambayo si halali kwenye ambako maji yatakuwa yanapita. Hivi sasa, maafisa wa kieneo wana changamoto ya fedha kuweza kushughulikia kurekebisha tatizo hili.”

Makaazi mbadala kwa raia

Serikali ya Zambia inasema inafanyakazi kuwapatia raia njia mbadala za makazi na kuondoa maji katika maeneo yaliyoathiriwa kote nchini.

Gabriel Pollen, mratibu wa Kitengo cha Utawala na Kupunguza Maafa nchini Zambia anasema mafuriko yamesababisha vifo vya watu wanane na takriban 373,000 wakiwa hawana makazi. Aliongezea kwamba mifugo milioni moja na nusu iliathiriwa, na magonjwa ya wanyama hivi sasa yameanza kusambaa.

“Katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa, tunaelewa vyema na dhahiri kwamba inafanya iwe vigumu kubashiri kiwango na ukubwa wa uharibifu ambao unaweza kutoka kutokana na hali mbaya ya hewa. Kwahiyo, kimsingi kinachotokea ni kuwashawishi watu kujenga maeneo ambayo ni thabiti na mbali na maeneo yanayoweza kuleta maafa, mbali na maeneo ya maji ya asili, mitiririko ya maji na mambo kama hivyo na kuwashawishi watu kujenga kwenye ardhi za nyanda za juu badala ya maeneo ya chini.”

Huku mvua nyingi zaidi ikitabiriwa, huenda ikawa ni muda mrefu kabla ya watu kama Chikwa kujenga nyumba mpya kwenye ardhi ya mwinuko na kuwaona watoto wake wakirejea shule.

XS
SM
MD
LG