Video kutokana na matukio hayo zinaonyesha maelfu ya watu wakishambulia majengo ya serikali, wakivunja madirisha, kupanda kwenye mapaa pamoja na kufanya uharibifu. Serikali imesema kwamba washukiwa hao watawajibishwa kwa mujibu wa sheria baada ya uchunguzi kukamilika.
Waziri wa sheria Flavio Dino amesema pia kwamba serikali inafanya uchunguzi ili kufahamu ni nani aliyegharamia mamia ya mabasi yaliyowasafirisha waandamanji kwenda Brasilia. Wafuasi wa Bolsonaro wanataka arejeshwe madarakani, na kulitaka jeshi kufanya mapinduzi.
Bolsonaro aliondoka Brazil kabla ya kuapishwa kwa rais wa sasa Luiz Inacio Lula da Silva wiki moja iliyopita. Kiongozi huyo sasa anaishi kwenye jimbo la kusini mwa Marekani la Florida. Rais wa Marekani Joe Biden amekemea tukio hilo akisema ni la kushangaza.