Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 20, 2024 Local time: 22:29

ICC yampa Bensouda wiki moja kumshitaki ama kumfutia mashitaka Kenyatta


Rais Uhuru Kenyatta alipofika mahakamani ICC kusikiliza kesi yake mwenzi Oktoba mwaka huu.
Rais Uhuru Kenyatta alipofika mahakamani ICC kusikiliza kesi yake mwenzi Oktoba mwaka huu.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imewapa waendesha mashitaka wiki moja kuongeza kasi ya uchunguzi ama kuyatupilia mbali mashitaka dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kesi imeahirishwa mara kadhaa na mahakama hiyo ya The Hague imetoa taarifa Jumatano ikisema kwamba kuchelewa zaidi kunaweza kuwa kinyume na maslahi ya haki katika mazingira haya.

Rais Kenyatta anakabiliwa na mashitaka dhidi ya ubinadamu akishutumiwa kupanga ghasia za baada ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2007 na mapema 2008. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 1,100 huko Kenya na kuwakosesha makazi wengine zaidi ya nusu milioni.

Rais Uhuru Kenyata anasema yeye hana hatia.

Upande wa utetezi unasema kesi dhidi ya rais Kenyatta imevunjika. Lakini waendesha mashitaka wanasema serikali ya Kenya imeweka vizuizi katika juhudi zake za kukusanya ushahidi ikijumuisha simu ya rais Kenyata, na kumbukumbu za kodi na benki.

Upande wa mashitaka umekiri kutokuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kiongozi huyo wa Kenya ikiwa utaendelea na kesi hiyo.

Mnamo mwezi Oktoba, bwana Kenyatta alikuwa rais wa kwanza aliyoko madarakani kwenda mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa, ambapo mahakama hiyo ilikuwa na kikao cha kuamua ikiwa itaendelea na kesi dhidi yake au itaifuta kesi hiyo.

Mkuu wa sheria huko Kenya bwana Githu Muigai alisema kuwa serikali imefanya kila jitihada kutimiza madai ya mahakama hiyo lakini akaongeza kwamba madai mengine kutoka kwa wendesha mashataka kamwe yasingetimilika.

Kesi dhidi ya rais Kenyatta inaonekana kama mtihani mkubwa kwa mahakama hiyo ya ICC, ambayo mpaka sasa imeweza kutoa hukumu mbili tangu ilipoanza kazi zake mwaka wa 2002.

Na ikiwa kesi hiyo itaendelea, bwana Kenyatta atakuwa rais wa kwanza aliyoko madarakani kushtakiwa katika mahakama hiyo.

Majaji Kuniko Ozaki, Robert Fremr na Geoffrey Henderson, walisema wanaacha mlango wazi kwa mwendesha mashtaka Fatou Bensouda, kufuta kesi dhidi ya rais huyo au kumshtaki upya kwa makosa yayo, hayo ikiwa atakuwa na ushahidi mpya katika siku za baadaye.

Lakini majaji hao walikataa ombi la Bensouda la kuiahirisha kesi hiyo bila kuwa na tarehe maalum ya kuirejelea. Bensouda alikuwa amewaomba majaji hao kumpa muda zaidi hadi serikali ya Kenya itakapompa rekodi zote anazoidai.

Hakuna tarehe mpya iliyotangazwa na majaji hao ya kusikiliza kesi dhidi ya rais huyo wa Kenya.

XS
SM
MD
LG