Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Mei 28, 2024 Local time: 04:47

Waziri wa Ulinzi wa Marekani atoa wito wa amani Mashariki ya Kati


Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alipokutana na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion huko Lod, Israel, Machi 9, 2023.REUTERS
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alipokutana na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion huko Lod, Israel, Machi 9, 2023.REUTERS

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin Al Hamisi alifanya mazungumzo nchini Israel huku wanamgambo watatu wa Kipalestina wakiuawa katika ghasia na jeshi la Israel pamoja na kuendelea kwa maandamano dhidi ya serikali yenye mrengo mkali wa kulia ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu

Netanyahu alilazimika kusafirishwa kwa helikopta hadi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa baada ya msafara wake kuzuiliwa na umati wa waandamanaji.

Maelfu ya Waisraeli wanaopinga mipango yenye utata ya mageuzi ya mahakama na sheria walifunga barabara ndani na karibu na uwanja wa ndege wa Ben Gurion, na mabadiliko ya dakika ya mwisho ilibidi kuchukuliwa ili kubadili mahala Austin alibidi kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel. Hali hiyo ikamulika kwenye jukwaa la kimataifa mgawanyiko wa kisiasa unaoendelea ndani ya Israel.

Na saa chache kabla ya Austin kuwasili, wanamgambo watatu wa Kipalestina waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa upelelezi wa polisi wa kulinda mpaka wa Israel katika Ukingo wa magharibi unaokaliwa, licha ya wito wa Umoja wa mataifa wa kutaka wimbi la ghasia linalolikumba eneo hilo mwaka huu lisitishwe.

Mkutano wa Austin na mwenzake Yoav Gallant ulihamishwa kutoka wizara ya ulinzi mjini Tel Aviv hadi karibu na uwanja wa ndege wa Gurion kutokana na maandamano makubwa kwenye uwanja wa ndege na karibu na wizara ya ulinzi.

Netanyahu alikutana pia na waziri wa ulinzi kwenye ukumbi huo huo, ofisi ya Netanyahu imesema.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mazungumzo yao kuanza, Netanyahu amesisitiza juu ya haja ya kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia "ajenda yetu ni moja, kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia na kuzuia uchokozi wa Iran, kudumisha usalama na ustawi wa kanda hii na kutafuta kupanua wigo wa amani. Na kwa ajenda hii muhimu, nina matarajio mazuri katika mazungumzo yetu" aliongeza Netanyahu.

Lloyd kwa upande wake amemwambia Netanyahu kabla ya mkutano wao kwamba Marekani inaendelea kuwa na dhamira ya kuhakikisha usalama wa Israel "uko sahihi, tuna mengi ya kuzungumza leo, na umesikia tukisema kila mara kwamba tuna dhamira thabiti kwa usalama wa Israel. Kwa hiyo, ninatarajia kuzungumzia mara kadhaa, mojawapo umeitaja hapo awali" aliongeza Lloyd.

Ziara ya Waziri wa ulinzi inafanyika wakati Israel inakabiliwa na changamoto hizo mbili maandamano na ghasia na hivyo Austin alichukua nafasi ya kuhimiza Israel kulinda misingi ya kidemokrasia na wakati huo huo kutoa wito wa kupatikana amani Mashariki ya Kati.

“Tunakutana leo wakati kuna hali ya mvutano. Tumefanya mazungumzo ya wazi kati ya marafiki kuhusu umuhimu wa kupunguza mivutano na kurejesha utulivu, hasa kabla ya likizo ya Pasaka na mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kama tunavyofanya siku zote, tunatoa wito kwa uongozi wa Palestina kupambana na ugaidi na kuanzisha tena ushirikiano wa kiusalama na kulaani uchochezi na kama ninavyofanya siku zote, nilikuwa wazi juu ya haki ya Israel kujihami dhidi ya ugaidi.”alisema Austin.

Maafisa wa usalama wa Israel wamesema walishambulia kijiji cha Jaba Kaskazini mwa Ukingo wa magharibi ili kuwakamata washukiwa wanaotafutwa kwa kushambulia wanajeshi wa Israel katika eneo hilo.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, maafisa wa usalama wa Israel wamewaua zaidi ya Wapalestina 70, wakiwemo wanamgambo wapiganaji na raia, katika kipindi hicho hicho, Wapalestina wamewaua Waisraeli 13 na mwanamke mmoja raia wa Ukraine katika mashambulizi yanayoonekana kuwa yalipangwa.

XS
SM
MD
LG