Qin ametoa wito huo katika taarifa iliyotolewa wakati alipokutana na mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika ambaye alieleza kusikitishwa na kile alichosema ni kutengwa kwa Afrika katika utawala wa kimataifa.
“Tunapaswa kuongeza uwakilishi na sauti za nchi maskini, hasa za Afrika, katika Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa,” Qin alisema wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa mjini Addis Ababa, kilichofadhiliwa na China.
Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Mahamat Faki amesema sio haki kuliona bara la Afrika halina kiti cha kudumu katika baraza kuu la dunia.
“Kwa miongo kadhaa sasa tumekua tukipambana kwa ajili ya mageuzi ya mfumo wa kimataifa kwa ujumla na hasa kwa niaba ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,” alisema.