Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed anasema anajiuzulu, akibadili ahadi aliyotoa wiki iliyopita kwamba ataendelea kubaki madarakani baada ya kuungwa mkono na Wasomali wanaopinga kuondoka kwake.
Waziri Mkuu Mohamed aliwaambia waandishi wa habari leo kuwa uamuzi wake wa kuwachia madaraka umechukuliwa kuepusha mgogoro wa kisiasa Somalia. Alisema kuondoka kwake ni kutokana na “maslahi ya watu wa Somalia.”
Alisema lakini ataendelea kubaki Mogadishu kuunga mkono juhudi za serikali mpya. Rais Sheikh Sharif Ahmed mara moja aliteua waziri mkuu wa muda ambaye atashikilia madaraka kwa siku 30.
Mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu ulitaka Bwana Mohamed kujiuzulu katika muda wa mwezi mmoja kufungua njia ya kuundwa kwa serikali mpya.