Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 09:42

Waziri avunja baraza la taifa la usalama barabarani Tanzania


Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, akizungumza katika eneo la ajali Mkoa wa Mbeya, Tanzania, Julai 05, 2018.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, akizungumza katika eneo la ajali Mkoa wa Mbeya, Tanzania, Julai 05, 2018.

Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na mabaraza yote ya ngazi ya mkoa nchini Tanzania yamevunjwa yakidaiwa kuwa yameshindwa kukabiliana na ajali za barabarani.

Vyanzo vya habari vimesema hatua hiyo imetangazwa Julai 5, 2018 na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alipokuwa akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mbeya.

Lugola ameeleza kuwa hajaridhishwa na utendaji wa baraza katika kukabiliana na ajali za barabarani.

“Nilikuwa namuuliza mwenyekiti wa baraza la usalama barabarani nikabaini hajui hata sheria inayoliweka baraza hilo n ahata kanuni zake hazijui, hii inaonyesha hatuna baraza na kuanzia sasa kwa mamlaka niliyonayo nalivunja baraza hili na nitaliunda upya,” amesema Lugola.

Amesema kutokana na ajali za barabarani, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kutekeleza hatua saba za kimkakati ili kukomesha ajali hizo.

Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa siku moja baada ya Rais John Magufuli kuagiza hatua zichukuliwe kudhibiti ajali mkoani Mbeya, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo imekutana kwa dharura kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo na kufikia maazimio sita ambayo yatasaidia kudhibiti ajali mkoani humo.

Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha ukaguzi wa magari na kufufua barabara ya zamani ya Mbalizi kama njia mbadala ya kupunguza madhara ya mtelemko mkali wa Mbalizi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari kikao hicho cha dharura chenye lengo la kutekeleza agizo la rais Magufuli, kamati hiyo ikiwa chini ya uenyekiti wa mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla imefikia maazimio sita yenye lengo la kukabiliana na ajali mkoani Mbeya.

Maazimio mengine ya kamati hiyo ni pamoja na kuwaondoa wafanyabiashara wote walio kwenye hifadhi ambao wako kwenye hatari ya kupata ajali.

Hatua nyingine ni kuwekwa kwa alama za barabarani kwenye maeneo yote zinapohitajika, ajenda ya usalama barabarani kuwa ya kudumu kwenye kamati za ulinzi za wilaya na pia kurekebisha miundombinu ya barabara katika maeneo yote hatarishi.

XS
SM
MD
LG