Afisa mmoja wa Sudan kusini amesema zaidi ya watu 3,000 wameuwawa katika mapigano ya kikabila yaliyozuka wiki iliyopita katika jimbo lenye mzozo la Jonglei.
Kamishna wa jimbo la Jonglei bwana Joshua Kronyi amesema miili ya wanawake 2,182 na watoto pamoja na wanaume 959 imehesababiwa hadi sasa.
Wiki iliyopita kundi la watu elfu sita wenye silaha kutoka kabila la Lou- Nuer lilivamia wajumbe wa kundi la kabila la Murle katika mji wa mbali wa Pibor. Wapiganaji walijiondoa wakati wanajeshi wa Sudan kusini walipofyatua risasi.
Alhamisi umoja wa mataifa ulisema unaongeza walinda amani wake katika mji wa Pibor kuhakikisha kuwa washambuliaji hawarejei tena katika kijiji.
Idadi ya majeruhi haijathibitishwa na maafisa wa jeshi la Sudan kusini au Umoja wa Mataif. Mkuu wa kikosi cha umoja wa mataifa cha ulinzi wa amani, Herve Ladsous amesema kwamba walinda amani katika eneo wameona dazeni kadhaa za miili ya watu.
Wengi wa maelfu ya wanavijiji waliokimbia mapigano wamerejea lakini wengi wanahitaji huduma za afya , chakula na maji.