Ghasia zilizoenea katika miji ya Misri ijumaa zimesababisha vifo vya watu watatu baada ya kuchochewa na zile ghasia za mauaji katika uwanja wa mpira.
Hasira dhidi ya vikosi vya usalama kushindwa kuzuiya ghasia jumatano zilizosababisha mkanyagano na kuuwa watu 74 zimepelekea maandamano ya kutaka utawala wa kijeshi kuachia madaraka kwa Serikali ya kiraia.
Milio ya bunduki , gesi ya machozi, mawe yaliyorushwa kwa polisi vilitawala hewani na kote katika uwanja wa kihistoria wa Tahrir huko Cairo ikifuatia na sala ya ijumaa.
Mamia ya waandamanaji waliokusanyika katika mitaa walikuwa wakiimba nyimbo za kupinga utawala wa kijeshi.
Daktari mmoja anayetibu waandamanaji karibu na uwanja huo aliliambia shairika la habari la Associated Press kwamba eneo lake la hospitali limejaa watu wengi waliojeruhiwa.