Siku mbili za mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Yemen na waasi wa kihouthi yamesababisha vifo vya watu 48 maafisa wa jeshi la Yemen walisema Jumapili.
Waasi wanaoungwa mkono na Iran katika mkoa kati ya majimbo ya Marib na Shabwa walipigwa na wanajeshi watiifu. Sitisho la mapigano kati ya majeshi ya Yemen na waasi kwa kiasi kikubwa lilikuwa linaendelea licha ya mapambano ya hapa na pale.
Sitisho la mapigano linalenga kufikia suluhisho la kudumu nchini Yemen wakati mazungumzo yanayofadhiliwa na Umoja wa Matiafa yakiendelea nchini Kuwait. Mapigano ya ardhini nchini Yemen pamoja na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia yamepelekea majanga ya kibinadamu, huku Umoja wa Mataifa ukisema asilimia 80 ya raia wa Yemen wanashida kubwa ya chakula na madawa.