Wataalam wa nishati ya umeme wanasema kuna mahitaji ya haraka ya uwekezaji binafsi na umma ili kufanikisha upatikanaji zaidi wa umeme barani Afrika. Wanasema serikali zinahitaji kufanya kazi na sekta binafsi ili kupunguza pengo la uzalishaji wa nishati hiyo.
Wakati nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zina rasilimali nyingi za kuwezesha uzalishaji wa umeme wa kutosha kama gesi, mafuta, makaa ya mawe, nishati asilia, jua, maji na upepo, wataalamu wa Benki ya Dunia wanasema Mwafrika mmoja kati ya watatu anaishi bila kupata huduma ya umeme. Stephen Njiru ni Mkurugenzi wa kampuni ya nishati asilia nchini Kenya, ya “Geothermal Development,” na mshauri wa mambo ya nishati wa rais. Anasema serikali zinapaswa kuweka sheria sahihi, mikakati na usimamizi, lakini bado zinahitaji ushirikishwaji wa sekta binafsi ili kufanikiwa.
Katika mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Washington wa kuiwezesha Afrika, Njiru anasema maafisa wanahitaji kutafakari njia thabiti ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, na wataalamu ili kuhudumia soko kubwa.
Nchi yake Kenya, ni moja ya nchi za mwanzo kushiriki katika mkakati wa ushirikiano wa Rais Barack Obama, wa “Power Africa,” kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme barani Afrika. Ushirikiano unazileta pamoja serikali za Afrika, makampuni binafsi, na idara za serikali ya Marekani.
“Powe Afrika,” imevutia uwekezaji wa sekta binafsi kwa zaidi ya dola bilioni 20 kwa ajili ya miradi mipya ya umeme. Andrew Herscowitz, mratibu wa Rais Obama, wa nishati na biashara kwa miradi ya Afrika, amesema amefurahishwa na mradi kama wa kampuni ya “Solar Reserve,” kampuni ya kimarekani yenye makazi yake Santa Monica, California, ambayo imeshinda zabuni ya kujenga mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 100 nchini Afrika Kusini.
Kampuni ya Kiholanzi na Marekani ya “Gigawatt Global,” imeanza kutekeleza uzalishaji umeme kwa kutumia jua nchini Rwanda. Herscowitz amesema mradi huo ni wa megawati 8.5 kwa maelfu ya watu. Kuna watu wengi ambao wanataka kuwekeza Afrika, ambao wana mawazo mazuri ya miradi ya nishati ya umeme.
Njia moja ya kuwezesha ushirika ni kuweka pande zote pamoja alisema Veronica Bolton Smith, ambaye ni meneja wa kuendeleza miradi wa kampuni ya “EnergyNet,” ambao waliandaa mkutano mjini Washington. Kwa hakika anasema, malengo ya mkutano ni kukumbusha wawekezaji na serikali kwamba kama unaweza kupata umeme, unaweza kusoma usiku, na kuweza kupika vizuri. Kuna mambo mengi yanaweza kufanikiwa kwa kupatikana kwa umeme kama kuongeza ajira, na hata kufanya sehemu za vijijini kuwa na umeme.
Lakini pamoja na yote hayo, kufanikisha hili si kazi rahisi. Balozi wa Tanzania, nchini Marekani, Liberata Mulamula, amesema serikali inahitaji usaidizi katika kukagua na kuchagua mapendekezo mengi.
“Unajua hawa wafanya biashara, wanacho kihitaji ni miradi, miradi, miradi. Na serikali zetu nyingi hazina uwezo mkubwa, tunahitaji fedha, lakini fedha kwa ajili ya miradi inayoaminika, hasa kama tunataka mabadiliko ya sekta ya nishati katika nchi zetu, tunahitaji ushiriki uliomakini, lakini pia ushiriki unaoratibiwa vizuri.” Alisema.
Anasema serikali nyingi zimegeukia taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Afrika, taasisi ya Millenium Challenge, na Benki ya Dunia, kwa utaalamu wa kusaidia nchi za Afrika, kuweza kuchagua miradi endelevu na inayowezekana kifedha.
Richard Bernard McGeorge, ni mtaalam kiongozi wa masuala ya fedha katika miundombinu wa Benki ya Dunia. Amesema kuongeza kasi ya uwekezaji binafsi, maafisa wa serikali wanapaswa kujiweka katika nafasi ya wawekezaji binafsi wa kifedha ambao mara zote wanataka uwazi, maono, na uwezekano wa marudio ili kuwekeza na si tu kwa mradi wa mtu binafsi bali pia kuwekeza tena katika nchi.
Wakati wataalam wa sekta hiyo wanasema soko la nishati barani Afrika linanufaika na ushiriki wa sekta binafsi, baadhi ya wawekezaji wanahofia gharama kubwa itawaweka kwenye wakati mgumu, majadiliano ya muda mrefu, na hali kubwa ya tahadhari. Lakini wataalam wa maendeleo na viongozi wa serekali za Africa, wanasema tahadhari ya kutowajibika ni kubwa, kuacha mamilioni ya watu bila umeme unaohitajika kuboresha maisha yao.