Takribani wataalamu 200 wa Ebola wanakutana huko Uswizi kuzungumzia uwezekano wa tiba na chanjo kwa ugonjwa huo, huku idadi ya kesi ikiendelea kuongezeka katika mataifa ya Afrika magharibi.
Shirika la afya duniani-WHO linasema mkutano huo wa siku mbili huko Geneva ni wa kutathmini maendeleo ya karibuni juu ya uwezekano wa matibabu kwa Ebola na kutaja hatua muhimu sana ambazo zinahitajika kuchukuliwa. Hakuna matibabu au chanjo kwa ugonjwa huu unaosababisha kifo, japokuwa dawa ya majaribio ya Zmapp, iliyotengenezwa na kampuni moja ya Marekani imetolewa kwa idadi ndogo ya wagonjwa, baadhi ya wagonjwa hao wamepona.
Mkurugenzi mkuu wa WHO, Margaret Chan alisema jumatano kwamba mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika mataifa ya Afrika magharibi hivi sasa umeuwa zaidi ya watu 1,900 na umewaambukiza watu wasiopungua 3,500, wengi katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.