Mashepe mkononi, wakazi wa majimbo ya mashariki mwa Marekani kuanzia Georgia hadi New York walitumia Jumapili kuchimbua theluji kutoka kando ya nyumba zao na magari baada ya zaidi ya mita moja ya theluji iliyosababishwa na dhoruba ya kihistoria kwa siku mbili nzima. Miji mingine iliyoko kaskazini mwa nchi kama Boston inajitayarisha kwa dhoruba hiyo ambayo tayari imeuwa watu wasiopungua 17.
Theluji ambayo haikuisha kasi hatimaye iliwacha kuanguka usiku wa Jumamosi, na kuacha watu wakihangaika na jinsi ya kurudi katika hali ya kawaida huku magari yakiwa yamefunikwa na theluji na njia za usafiri wa umma kufungwa tangu Ijumaa jioni.
Viwanja viwili vya ndege vikubwa katika eneo la Washington, Uwanja wa Kimataifa wa Dulles na Reagan National, viliendelea kufungwa Jumapili huku wafanyakazi wakiondoka theluji katika njia za ndege.
Wataalam wa hali ya hewa wanasema dhoruba hiyo imeshika nafasi ya tano katika orodha ya dhoruba mbaya za theluji zilizowahi kupiga eneo hili.
Katika mwambao wa mashariki, Idara ya hali ya hewa ya taifa inasema bustani maarufu ya jiji la New York, Central Park, ilirekodi sentimita 64 za theluji. Jumpili asubuhi maafisa waliondoa marufuku ya kusafiri ambayo ilikuwa imezuia wakazi millioni nane na nusu wa mji huo kwenda popote tangu Jumamosi.
Maeneo ya pwani kutoka Virginia hadi New Jersey pia yalipata mafuriko kutokana na dhoruba hiyo.
Kiasi cha watu millioni 85 waliathirika na dhoruba hiyo, na maelfu kwa maelfu wangali hawana umeme wakati maelfu wengine walikwama mabarabarani au kutoweza kuanza safari zao baada ya njia nyingi za usafiri kufungwa katika mwambao mzima wa pwani ya mashariki.
Watu wasiopungua 17 wamefariki kuanzia Georgia hadi New England. Majimbo kumi yalitangaza hali ya dharura. Katika jimbo la Kentucky, maafisa walifungua maeneo ya hifadhi ya dharura kando kando ya barabara kuu ya jimbo baada ya watu kukwama kwenye magari yao kwa saa zisizopungua 10
Mafuriko mwambao wa Jersey
Maji yaliyojaa katika bahari ya Atlantic yalienea katika mitaa ya miji iliyopo eneo la pwani, ikichanganyika na theluji na kujaa katika maeneo ya nyumba za watu Jumamosi. Hata hivyo, wasiwasi mkubwa uko katika wingi wa theluji ambayo nayo inaweza kusababisha ongezeko la mafuriko.
Gavana wa New Jersey Chris Christie alilazimika kuwacha kampeni yake ya kuwania ugombea urais kwa chama cha Republican na kurudi nyumbani kusimamia shughuli za kuondoa theluji na kusaidia walioathirika.