Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 22, 2024 Local time: 15:24

Wangari Maathai kuzikwa Jumamosi


Wangari Maathai, mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2004
Wangari Maathai, mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2004

Familia ya Wangari Maathai imesema mwili wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel utachomwa moto Jumamosi nchini Kenya

Familia ya Wangari Maathai wa Kenya imetangaza mwili wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2004, utachomwa moto mjini Nairobi, Jumamosi.

Msemaji wa familia, Vertistine Mbaya alisema Jumatatu kuwa hatua za uchomaji moto ni kwa mujibu wa ridhaa ya Maathai. Sherehe za upandaji miti pia zitafanyika Jumamosi, kukumbuka mchango wake wakati wa uhai wake.

Maathai alikuwa mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya amani ya Nobel. Alikufa akiwa na umri wa miaka 71, Jumapili iliyopita baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.

Maathai alishinda tuzo ya Nobel kwa jitihada zake dhidi ya serikali ya zamani ya mabavu ya Kenya na kazi yake ya kuboresha maisha ya wanawake.

Alianzisha taasisi ya Green Belt Movement, ambayo iliwasaidia wanawake maskini wa vijijini kupitia program ya upandaji miti iliyobuniwa kutoa huduma za msingi kama vile kuni, chakula na maji safi ya kunywa. Taasisi hiyo inasema ilihamasisha maelfu ya wanaume na wanawake kupanda zaidi ya miti milioni 47.

Taasisi hiyo ilipanuka na kuhamasisha masuala mengine kama vile demokrasia, haki za binadamu, haki za wanawake na amani.

Maathai pia alihudumu kama mwakilishi katika bunge la Kenya na naibu waziri wa mazingira nchini humo.

Maathai alipata elimu ya juu katika chuo kimoja nchini Marekani wakati wa enzi za haki za kiraia katika miaka ya 1960 na alisema kwamba uzoefu huo ulimhamasisha yeye kurudi nyumbani na kufanya mambo mazuri kwa watu wa Kenya.

XS
SM
MD
LG