Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Februari 11, 2025 Local time: 02:32

Wanawake wa Kimasai wanavyopambana na mila zinazowagamdamiza


Wanawake wa Kimasai huko Tanzania. Decemba 14, 2024. Picha na REUTERS/Onsase Juma.
Wanawake wa Kimasai huko Tanzania. Decemba 14, 2024. Picha na REUTERS/Onsase Juma.

Jamii ya wanawake wa Kimasai nchini Tanzania imeendelea kupambana na changamoto mbalimbali za kimila na kijamii katika harakati za kupata elimu, licha ya muamko unaoonekana miongoni mwao juu ya umuhimu wa elimu.

Ndoto za wasichana wengi bado zinatatizwa na mila kandamizi kama ndoa za utotoni, ukeketaji, ukosefu wa miundombinu, Pamoja na shinikizo la kuendeleza majukumu ya kijadi.

Jamii hiyo ya wanawake wa kimasai imekuwa jamii maarufu kwa kutunza na kuhifadhi tamaduni zake kwa miaka migi huku kwa hivi sasa wanawake katika jamii hiyo wameanza kupata muamko juu ya umuhimu wa elimu huku wakielendelea kuweka kipaumbele katika kutunza tamaduni zao.

Licha ya kuwepo kwa muamko huo ndoto za wanawake wengi katika jamii hiyo zimeendelea kukumbana na changamoto mbalimbali katika utafutaji wa elimu ikiwa ni pamoja na uchache na umbali wa shule katika maeneo ya jamii hizo kama anavyoeleza.

Akizungumza na Sauti ya Amerika, Denis Oleshangai Wakili wa kujitegemea huko Arusha amesma “watoto wa kike wanakumbana na hiyo changamoto sana ya umbali wa shule na uchache wa shule”

“kwa mfano unaweza ukakuta kwamba kijiji kimoja kina shule moja au unakuta hata hakuna shule kabisa kwahiyo mtu inabidi usafiri karibia kilomita sita kufuata shule na wakati fulani pia kunakuwa na mito na wanyama wakali” ameongeza.

wasichana wa Kimasai huko Kilimanjaro Tanzania. Picha na Reuters
wasichana wa Kimasai huko Kilimanjaro Tanzania. Picha na Reuters

Changamoto za kimila nazo zimeendelea kukwamisha ndoto za wanawake wengi, Mila hizo ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, watoto wa kike kutokupewa

kipaumbele katika elimu, shinikizo la kijamii la kuendeleza majukumu ya kijadi, pamoja na ukeketaji ambao umekuwa chanzo kikuu cha mimba za utotoni.

Nailejileji Asia Tipap Mtetezi wa haki za wanawake katika jamii za asili amewataka viongozi wa kimila kuendelea kutumia tamaduni nzuri na mikusanyiko ya kimila kutoa elimu kwa jamii ya kimasai juu ya umuhimu wa elimu na umuhimu wa kuacha mila kandamizi dhidi ya mtoto wa kike.

“Kupitia zile tamaduni zetu nzuri tuendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wake kwa watoto wote, tuna sikukuu nyingi kama jamii hii mikusanyiko ya kwetu kama jamii viongozi wetu wa kijamii waendelee kutumia maeneo hayo kutoa elimu na kutoa hamasa kwa jamii juu ya suala la elimu” amesema Asia.

Asia ameongeza kuwa juhudi za viongozi wa kimila zinapaswa kuungwa mkono na jamii nzima, hususan wale wenye uelewa juu ya athari za mila kandamizi. amesema kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya wazazi, viongozi wa kimila, na mashirika yanayotetea haki za wanawake unaweza kusaidia kufanikisha mabadiliko ya mtazamo kuhusu nafasi ya mtoto wa kike katika jamii.

Aidha, ametoa wito kwa wanawake wanaopata fursa ya elimu kutoka katika jamii hizo kujenga utamaduni wa kurudi katika jamii zao ili kutoa elimu na kuwahamasisha watoto wa kike. Kwa kufanya hivyo, amesema, wanawake watakuwa sehemu ya suluhisho katika kupambana na changamoto zinazowakabili watoto wa kike.

Nae Naseko Nenye mkazi wa Kilimanjaro, anaongezea kuwa kutokana na kukosekana kwa elimu inapelekea wanawake wengi kutokuruhusiwa kushiriki katika shughuli za kijasiriamali hali inayoathiri maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.

Rais wa Marekani George W. Bush alipoitembelea shule ya wasichana wa Kimasai huko Arusha, Tanzania Februari 18, 2008. Picha na Reuters.
Rais wa Marekani George W. Bush alipoitembelea shule ya wasichana wa Kimasai huko Arusha, Tanzania Februari 18, 2008. Picha na Reuters.

“Suala kubwa ni kutokuruhusiwa kujishughulisha lakini pia hata wanaoruhusiwa kujishughulisha hawana chanzo cha pesa, wanataka kujishughulisha labda wanataka kuanzisha biashara lakini hawana pakupata hiyo mitaji” amesema Masai.

“wengine wana mitaji na hawaruhusiwi kwenda kufanya sababu wanasema wanawake wapo kwaajili ya kule na sio kwaajili ya kutafuta” ameongeza.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Sebastian Kitiku amesema serikali inaendelea kufanya jitihada za kujenga shule katika maeneo ya jamii za wafugaji ili kuhakikisha jamii hizo zinapata elimu kwa ubora zaidi.

“Serikali inafanya juhudi kubwa ukiangalia hivi karibuni tumejenga shule nyingi ambazo zinawalenga watoto wa kike katika makabila kama ya wamasai wanao hama mara kwa mara kwahiyo ni mkakati wa serikali kuhakikisha kwamba kunakuwa na shule za kutosha katika maeneo ambayo yana jamii za wafugaji lakini vilevile wale wanaoendekeza ukatili dhidi ya watoto kama kuwaoza na kuwakeketa sheria zipo wazi” amesema Kitiku.

Aidha mkurugenzi huyo amesema serikali inaendelea kufanya maboresho ya sheria ili kuhakikisha kuwa wanawake wanaendelea kulindwa na kuhakikisha kuwa haki za wanawake zinasimamiwa.

Imatayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG