Takriban wanachama 23 wa kikosi kazi cha pamoja cha raia nchini Nigeria waliuawa Jumamosi katika mashambulizi tofauti yaliyofanywa na wanamgambo pamoja na genge la utekaji nyara lenye silaha kaskazini mwa Nigeria, maafisa wawili kutoka kikosi cha jeshi wamesema leo Jumapili.
Katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno, kitovu cha uasi wa Ki-islamu, wapiganaji wanaoshukiwa kuwa wa Islamic State West Africa Province (ISWAP) walitumia kifaa cha milipuko (IED) kulipua gari lililobeba Civilian Joint Task Force (CJTF), mwenyekiti wa kikosi katika eneo hilo alisema.
CJTF iliundwa kwa mwaka 2013 ili kuzilinda jamii kaskazini mashariki na kulisaidia jeshi kupambana na Boko Haram na baadaye kuitokomeza ISWAP. Kikosi hicho tangu wakati huo kimepanuka hadi katika majimbo mengine ya kaskazini ambayo yanakabiliana na magenge ya utekaji nyara yenye silaha.
Tijjanima Umar, mwenyekiti wa CJTF katika eneo la Gamboru Ngala karibu na mpaka na Cameroon, alisema timu yake ilikuwa ikisafiri kwenda mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri wakati gari lilipokanyaga kilipuzi kilichotegwa barabarani IED.
Wakati kilipuzi kilipolipuka watu tisa kati yao walikufa hapo hapo, wakati wengine wawili walipata majeraha makubwa na haraka walikimbizwa hospitali kwa matibabu, Umar aliliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu. Jeshi la Nigeria halikupatikana mara moja ili kutoa maoni yake.
Ingawa wamezuiliwa kwa kiasi kikubwa na vikosi vya usalama vya Nigeria, Boko Haram na ISWAP bado wanafanya mashambulizi yanayosababisha vifo dhidi ya raia na jeshi.
Forum