Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 05:02

Wakongo wafurahia kujisalimisha kwa Ntangada


watu walopoteza makazi yao mashariki ya Congo wakisubiri kupata chakula kutoka kwa Idara ya Chakula Duniani WFP, August 8, 2012.
watu walopoteza makazi yao mashariki ya Congo wakisubiri kupata chakula kutoka kwa Idara ya Chakula Duniani WFP, August 8, 2012.
Wakongomani wameridhika na kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda kwenye ubalozi wa Marekani mjini Kigali, lakini wajiuliza ikiwa kweli atafikishwa mahakamani.

Serikali ya Kongo imeiomba Marekani na Rwanda kurahisisha kupelekwa kwa Ntaganda mbele ya mahakama ya ICC, huku mashirika ya kiraia na yale ya kutetea haki za binadamu yakiomba kutendewa haki kwa wahanga wa machafuko ya Kivu na Ituri.

Swali kubwa ambalo wakazi wa Kinshasa wamejiuliza siku ya Jumanne siku moja baada ya Ntangada kujisalimisha, ni ikiwa mtuhumiwa huyo wa uhalifu dhidi ya binadamu atapelekwa mbele ya mahakama ya ICC ama la.

Baadhi ya wakazi wa Kinshasa tuliozungumza nao bado hawajaamini kujisalimisha kwa Ntaganda, mfano wa Jean Paul Muiti ambaye ni mzaliwa wa Kivu na aliyekimbia vita vya mwaka 2008 baina ya jeshi na waasi wa CNDP, na hivi sasa anaishi mjini Kinshasa , amesema kujisalimisha kwa Ntaganda siyo suluhisho la mgogoro wa Kivu.

Serikali ya Kongo imeelezea kwamba kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda ni hatua kubwa katika juhudi za kurejesha amani na usalama wa Kivu.Waziri wa habari na msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende amesema kuwa Marekani na Rwanda wanamajukumu ya kurahisisha kufikishwa kwa Ntaganda kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC :

Afisi ya Umoja wa Mataifa inayoshugulikia amani nchini Congo,Monusco imeomba pia Ntaganda apelekwe ICC katika muda usiyo mrefu.Msemaji wa Monusco,Carlos Araujo amesema Bosco Ntaganda anatuhumiwa kwa makosa mengi ya uhalifu :

“Monusco imeunga mkono juhudi zote zinazofanywa hivi sasa ili Ntaganda afikishwe mahakamani.Monusco inategemea pia kwamba kusafirishwa kwa Ntaganda kwenye mahakama ya ICC kutamaliza kutotolewa adhabu ambako alifaidika kwa muda mrefu”.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya hapa nchini yamepongeza kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda na kuomba haki itendewe kwa maelfu ya wakaazi wa Kivu na Ituri waliothiriwa na ubabe wa Ntaganda.Huko Ituri, Mitterand Bosa ni katibu mtendaji wa shirika la JusticePlus.

“Kulikuwa na waathiriwa wengi, kuna watu wengi waliouwawa ,wanawake waliobakwa kufuatia ubabe wa Bosco Ntaganda.Kwetu sisi ni furaha sana kumuona Bosco amehukumiwa na kwa hiyo tumeomba apelekwe ICC haraka iwezekanavyo”.

Ikiwa wengi wamefurahia kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda ,lakini wadadisi wa maswala ya siasa wamehisi kwamba kufikishwa kwa Bosco Ntaganda kwenye mahakama ya kimataifa kumewatia wasiwasi mwingi viongozi wengi wa Rwanda, Congo na Uganda ambao kwa namna moja ama nyingine walimpa Ntaganda msaada wa hali na mali ili kuendesha ukatili wake kwa maslahi yao.
XS
SM
MD
LG