Wakazi kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba walirejea mitaani Jumanne wakati wa usitishaji mapambano ya siku tano yaliyosababisha vifo vya karibu watu 200.
Lakini wakazi wengi waliotembelea soko kuu la Juba wakitafuta chakula walishtuka kukuta maduka yaliyoporwa vitu na bei za vitu kuwa juu kutokana na upungufu wa bidhaa. Wachuuzi katika soko la Jebel waliwasili mapema Jumanne na kukuta maduka na bidhaa kwenye meza zao zimeibiwa.
Mfanya biashara Aziz Francis alisema duka lake lina thamani ya kiasi cha dola 33,000 kila kitu kiliibiwa wakati wa mapigano. Aliwalaumu wanajeshi ambao walipangiwa kulinda eneo la soko.
Francis alisema duka hilo ndio chanzo chake cha mapato pekee alichonacho. Alisema ana khofu kuhusu namna atakavyomsaidia mke na watoto wake watatu na namna atakavyoweza kulipa ada za shule za watoto wake.