Italy inasema meli za uokozo zinazofanya shughuli zake pwani ya Libya ziliwaokoa zaidi ya wahamiaji 2,500 kwa salama siku ya Jumatatu na inasema idadi yao inaongezeka wakati hali ya hewa inaimarika katika Mediterranean.
Walinzi wa pwani wa Italia walisema wahamiaji kamili 2,000 walivutwa kutoka kwenye boti ndogo na boti moja kubwa. Taarifa ilisema meli za majini za Ireland na Malta, sehemu ya jeshi la kimataifa linaloangalia kuzuia uzamaji mkubwa unaotokea kwenye bahari liliwaokoa mamia wengine na kwamba meli ya mizigo iliyokuwa ikipita pia ilijumuika na juhudi za uokozi.
Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya wahamiaji 3,000 wengi wao kutoka kusini mwa jangwa la Sahara wameokolewa kutoka bahari ya Mediterranean na kupelekwa kwenye vituo vya wakimbizi nchini Italy kwa mwaka huu.
Maafisa wa masuala ya haki za kibinadamu wanasema njia ya bahari kutoka Libya kwenda Italy hivi sasa imekuwa njia kuu kwa wahamiaji wanaoelekea ulaya baada ya mkataba wa karibuni kati ya umoja wa ulaya-EU na Uturuki kupunguza mtiririko wa wahamiaji kutoka pwani ya Uturuki kwenda Ugiriki.