Wagombea 12 wa Kongo wamewasilisha fomu zao kwa ajili ya kuwania kiti cha rais kwenye uchaguzi wa Novemba 28 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, siku ya Jumatatu mjini Kinshasa. Rais Joseph Kabila pia alirejesha fomu yake siku ya Jumapili ilikuwania kwa muhula wa pili
Upinzani wa Kongo umeshindwa kuafikiana ili kumpata mgombea mmoja. Daftari ya dharura ya wagombea baada ya kuchunguzwa kwa fomu zao na tume huru ya uchaguzi itatangazwa mnamo kipindi cha siku tano zijazo.
Wagombea hao ni pamoja na Anti Passi Mbusanya Mwisi ambaye mpaka Jumapili alikuwa waziri wa miji na mitaa katika serikali ya Kabila kabla ya kufukuzwa kazi. Mgombea mwingine ni Nzanga Mobutu mtoto wa dikteta Mobutu Seseko ambaye naye alikuwa naibu waziri mkuu kabla ya kufukuzwa kazi mwezi Machi iliyopita.
Mkongwe wa siasa nchini DRC Etienne Tsisekedi mwenye umri wa miaka 79 anachukuliwa kuwa mmoja kati ya wapinzani wakuu wa Kabila kutoka jimbo la Kasai. Pamoja na Vitali Kamere, mgombea mashuhuri wa Kivu Kusini mwenye umri wa miaka 52 aliyekuwa spika wa bunge na alijiunga na upinzani mwaka jana baada ya kutofautiana na rais Kabila.
Wagombea wengine ni spika wa sasa wa baraza la Seneti kutoka jimbo la Equatorial Leon Kengo wa Dondo (76) aliwahi kuwa waziri mkuu wa Mobutu kwa miaka 8. Na kutoka jimbo la Kasai ni Oscar Kashala ambaye ni daktari anayeishi Marekani yeye pia aliwahi kugombea mwaka 2006.
Upande wa chama cha MLC hakikutaja mgombea wake lakini kiongozi wa chama hicho Kinshasa Adam Bombole amejitaja kuwa mgombea huru yeye ni mfanyabiashara mkuu ana umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.
Naye mwanamke pekee katika uchaguzi huo ni Bibi Bernadette Nkoimafuta ambaye ni mfanyakazi wa zamani wa Umoja wa Mataifa lakini hafahamiki na wengi nchini humo. Wengine ni pamoja na Ismail Kitenge, Sifor Kakese na Jean Ande Kajamba.