Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 22:51

Waathirika wa fistula wapewa matibabu na mafunzo ya ufundi stadi Tanzania


Baadhi ya wanawake waliopata matibabu ya Fistula wakiwa darasani katika hospitali ya CCBRT Tanzania. Picha na VOA
Baadhi ya wanawake waliopata matibabu ya Fistula wakiwa darasani katika hospitali ya CCBRT Tanzania. Picha na VOA

Wanawake Tanzania waliopona baada ya kupatiwa matibabu ya fistula sasa wanapewa mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujitegemea kimaisha wanaporudi katika familia zao.

Wanawake hao ambao hapo awali walitengwa na jamii kutokana na maradhi hayo, wanapatiwa mafunzo ya ufundi stadi yanajumuisha ushonaji, ufumaji, na ujasiriamali, yakiwa na lengo la kuwapa wanawake hao ujuzi utakaowasaidia kujipatia kipato na kujenga maisha mapya.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika Sophia Nandonde, mkazi wa Dar es Salaam, amesema kuwa baada ya kupatiwa matibabu ya fistula, ndoto yake sasa ni kufungua kituo cha mafunzo ya kushona nguo. Kupitia kituo hicho, anatarajia kupata kipato kitakachomsaidia kuendesha maisha yake.

“Nikitoka hapa nakwenda kuwa fundi na nitakuwa mwalimu, najua lazima nitapata wanafunzi kwa mafunzo niliyo yapata najua mtaani sio wengi sana wanaoshona mabegi kwahiyo nikirudi kule nitakwenda kuwa fundi mzuri na wanafunzi nitawapata najua nitapata hela kupitia wanafunzi wangu,” alisema Nandonde

Sophia Nandonde akiwa darasani akipata mafunzo katika hospitali ya CCBRT iliyoko jijini Dar es Salaam. Picha na VOA
Sophia Nandonde akiwa darasani akipata mafunzo katika hospitali ya CCBRT iliyoko jijini Dar es Salaam. Picha na VOA

Kwa mujibu wa hospitali ya CCBRT imefanya upasuaji kwa akina mama 1,350 wenye fistula kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, huku kwa kipindi cha miezi minne ya kwanza ya mwaka huu pekee, jumla ya wagonjwa 126 wa fistula wamefanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo.

Mwanahamisi Ally ni miongoni mwa wanawake hao walionufaika na mafunzo hayo, amewataka wanawake wanaokutwa na changamoto ya fistula wasiope kujitokeza kwa kuwa matibabu yanapatikana na pia unapata nafasi ya kupata mafunzo ya ujasiriamali.

“Wanawake wenzangu wanaopitia changamoto ya kuwa na fistula wasijisikie vibaya kuanzia sasa hivi wawe huru kwasababu matibabu yapo muda wote unapokelewa vizuri na maisha yako yanaenda vizuri kama hivi unakuja kutibiwa ukisharudi ndio hivyo unapigiwa simu tena unakuja kwenye mafunzo kwahiyo maisha yako yatakuwa sawa.” Alisema Ally.

Hata hivyo Suzani Tabura ambaye ni mkufunzi kutoka mabinti Centre ameeleza kuwa baada ya wanawake hao kupata matibabu na mafunzo bure pia vile vile wanapatiwa mitaji ya biashara, cherehani pamoja na malighafi za kwenda kuanzishia ufundi wao.

“Mafunzo haya ya ujasiriamali yanatolewa bure kwa wale ambao tumepona fistula na baada ya kumaliza haya mafunzo tunapatiwa mitaji bure kwaajili ya kwenda kuanza biashara,” alisema Tabura.

“Tunapatiwa pia cherehani ya kufanyia kazi tunapatiwa pia malighafi kwaajili ya kuanzia biashara wewe mwenyewe nyumbani.” aliongeza.

Maadhimisho ya siku ya fistula kwa mwaka 2024 yamebeba kauli mbiu inayosema "Vunja mnyororo tokomeza fistula" ikitoa wito kwa wanawake kujitokeza wanapopata changamoto hiyo ili waweze kupatiwa matibabu.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG