Waasi wa Libya wanasema wamekamata kituo muhimu kwenye mpaka wake na Tunisia, lakini mapigano bado yanaendelea kupata udhibiti wa mji wa magharibi wa Zuwarah.
Wapiganaji wa upinzani wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa majeshi yanayomtii Moammar Gadhafi katika juhudi zao za kusonga mbele kuingia Zuwarah. Ni sehemu muhimu ya kupitisha bidhaa kwenda Tripoli. Mji huo wa pwani uko kiasi cha kilometa 50 kutoka mpaka wake na Tunisia.
Siku ya Ijumaa, waasi walikamata kituo cha mpakani cha Ras Adjir kwenye njia hiyo hiyo.
Wakati huo huo, ndege za kivita za NATO zimepinga handaki kubwa katika mji aliotoka bwana Gadhafi wa Sirte hapo jana. Kiongozi wa Libya hajasikika wala kuonekana tangu waasi waikamate Tripoli; Sirte unadhaniwa ndiyo sehemu aliyokwenda kujificha.
Ndege za kivita za Uingereza zimefyatua makombora kwenye eneo la handaki huko Sirte. Waziri wa Ulinzi wa Uingere, Liam Fox amesema NATO haimlengi bwana Gadhafi, lakini mashambulizi ya anga yana azma ya kuhakikisha kuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, na majeshi yake kamwe hawaendelezi vita.
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, katibu mkuu Ban Ki-moon amesema kwamba taasisi za Afrika, Arabuni na Ulaya zimekubaliana kwamba mzozo wa Libya umeingia katika awamu mpya. Bwana Ban amesema jumuiya ya kimataifa iko tayari kupeleka jeshi la polisi huko Libya, kama wakiombwa, kwasababu nchi hiyo imejaa silaha ndogo ndogo.