Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Septemba 15, 2024 Local time: 04:09

Waandishi wa habari Kenya wakhofia utendaji kazi wao


Oscar Obonyo, Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Kenya-KUJ
Oscar Obonyo, Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Kenya-KUJ

Maoni na hisia mbali mbali zimetanda nchini Kenya kufuatia hatua ya Bunge la Taifa ya kupitisha mswaada wa sheria wenye nia ya kuwaadhibu waandishi wa habari wanaotangaza au kuchapisha habari zisizo-wafurahisha wabunge. Hii ni mara ya pili kwa bunge la taifa mjini Nairobi kupitisha mswaada wa sheria wenye nia ya kuwachukulia hatua kali waandishi wa habari.

Iwapo Rais Uhuru Kenyatta ataidhinisha mswaada huo wa sheria, hii ina maanisha kwamba waandshi wa habari nchini Kenya watakuwa hatarini kwa sababu watachukuliwa hatua kali ya kisheria wakiandika habari zisizo-wapendeza wanasiasa na hasa wabunge.

Kulingana na mswaada huo wa sheria, mwana-habari atakayepatikana na hatia ya kuchapisha au kutangaza habari zisizo sahihi kuhusu maswala ya Bunge, huenda akatozwa faini ya shillingi laki tano au kifungo cha miaka miwili jela au adhabu zote mbili zikiandamana pamoja.

Hata hivyo baraza kuu la waandishi wa habari pamoja na makundi ya kidini yamepinga vikali mswaada huo wa sheria. Pia wananchi wa kawaida wamekasirishwa na msaada huo.

Mswaada kama huo ulikuwa umewasilishwa hapo awali lakini Rais Uhuru Kenyatta alikataa kutia saini mswaada huo.

Taarifa iliyotolewa na viongozi wa kidini inapinga vikali mswaada huo na kudai shabaha yake ni kuwazuia waandshi wa habari kuangazia maovu na kashfa mbali mbali zinazowahusu wabunge pamoja na utovu wa nidhamu katika bunge.

Bunge la Kenya
Bunge la Kenya

Jambo la kushangaza ni kwamba mswaada huo uliungwa mkono na wabunge wote wale wa mrengo wa serikali na upinzani.

Lakini Senator wa Mombasa, Omar hassan alisema sheria hiyo ni ya kujitakia makuu kwa wabunge na kama ni wakati wa enzi ya Rais Moi, mswaada huo ungepita kwa urahisi.

Kwa hivi sasa chama kikuu cha wana habari kimewasilisha malalamiko yake kwa Baraza la Senati kikitarajia kwamba baraza hilo litapinga mswaada huo.

XS
SM
MD
LG